The House of Favourite Newspapers

TUKIWAPENDA WASIOTUPENDA, TUWE TAYARI KULIA!

HAKUNA shaka tulio wengi tupo katika uhu­siano wa kimapenzi wa mashaka. Hakuna hata mmoja wetu ambaye anaweza kujiamini­sha kwa asilimia mia moja kwamba mpenzi wake aliye naye an­ampenda kwa dhati kabisa au anazuga. Hii inabaki kuwa siri ya anayependa! 

 

Lakini sasa, kuna kitu nilichogundua miongoni mwetu, kitu ambacho tusipokuwa makini nacho tunaweza kujikuta tuna­jilazimisha kuishi maisha ya huzuni wakati tunayo haki ya kuishi maisha ya yenye furaha. Ukweli ni kwamba, kila mtu anao uhuru wa ku­penda kwani maisha bila mapenzi lazima yatakuwa na kasoro.

 

Lakini sasa, uhuru huo usikufanye ukalazimika kumpenda mtu ambaye anaonesha wazi kuto­kuwa na mapenzi kwako. Hivi utampendaje mtu ambaye hakupendi? Sawa, huwezi kujua kwamba hakupendi kwani huwezi kuufungua moyo wake lakini, kuna dalili za wazi zinazoweza kukudhihirishia kuwa, mtu huyo anakuzingua tu na kutaka kukupotezea muda wako.

 

Kitu kinachoniuma na ambacho ndicho kilinisu­kuma kuandika makala haya ni tabia ya baadhi ya watu kung’ang’ania wa­naume ambao wanaone­sha kabisa kutowap­enda, ukimuuliza kwa nini anamng’ang’ania wakati hapati anachokitaka, anakuam­bia eti anampenda sana.

 

Jamani ifike wakati tutambue kuwa, kutokea kumpenda mtu na yeye akakupenda kwa dhati ni bahati sana. Wengi wetu tunatokea kuwapenda watu wasiotupenda, matokeo yake ni kuumizwa kila wakati.

 

Wewe jaribu kuchunguza utabaini walio wengi hawapati mapenzi wanayoyatarajia kuto­ka kwa wapenzi wao badala yake huishia kilizwa kila mara. Niseme tu kwamba, ka­nuni ya mapenzi inasema, nipe nikupe, nipende nikupende, niheshimu nikuheshimu.

 

Kama unabaini dalili f’lani f’lani za wazi kwamba mpenzi wako hakupendi, usijilazimishe kuendelea kumpenda. Ukifan­ya hivyo utamfanya aendelee kuku­nyanyasa kwa kuwa anajua umeoza kwake na huwezi kumuacha. Huenda wewe unayesoma makala haya sasa hivi unajiamini sana kwamba mpenzi wako ana­kupenda, hiyo ni nzuri na ndivyo ambavyo kila mtu anatakiwa kuishi.

 

Tambua kuwa na imani kwamba mpenzi wako anakupenda ndiko kutakufanya uishi maisha ya furaha na amani huku na wewe ukijita­hidi kuonesha kumpenda kwa dhati, hapo mtaishi. Lakini kama unaona penzi la mpenzi wako ni la mashaka ni wakati wako sasa wa kufanya maa­muzi sahihi huku ukiamini kwamba bila yeye unaweza kuishi.

 

Kumbuka kauli ya ‘siwezi kuishi bila yeye’ ni ulim­bukeni kabisa tena watu wakikusikia unasema hivyo watakuona ni mshamba wa mapenzi. Mambo hayo yamepitwa na wakati Kimsingi una­takiwa kuwa na moyo wa ujasiri kwamba, kama yeye analidharau penzi lako wapo wanaolitafuta kwa udi na uvumba na huenda huyo uliye naye anaku­wekea kauzibe tu. Hebu jaribu kupingana na mawazo haya na ujiweke huru.

 

Ukweli unabaki palepale kwamba, kumuacha mtu ambaye ulitokea kumpenda sana si kazi ndogo. Ni kazi inayo­hitaji ujasiri wa hali ya juu. Ifike mahali basi useme, inatosha na amua kumuacha. Potelea mbali ili mradi upate uhuru wa kuishi mai­sha ya raha mustarehe. Amini kuwa, huenda Mungu hakukupangia ufurahie maisha na huyo uliye naye sasa kwa kuwa yule wako ali­yekupangia yuko njiani na utasahua maumivu yote.

Stori: Amran Kaima

Comments are closed.