The House of Favourite Newspapers

Tukutane tena wiki ijayo! Kuelekea kuuaga mwaka 2016, unalitathiminije penzi lenu?

couple-wapendanao-mahabaUmebaki muda mfupi kabla ya kuuaga Mwaka 2016 na kuingia Mwaka Mpya wa 2017! Ni suala la kila mmoja wetu kuendelea kumuomba Mungu atuvushe salama kwani wapo wengi waliotamani kufika lakini mpaka leo hatunao tena.

Mimi na wewe ambao bado tunapumua, hatuna budi kumshukuru Mungu na kuendelea kumuomba atuvushe salama kuingia mwaka mpya.

Karibu tena tujadili mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi. Njia nzuri ya kuuaga mwaka huu na kujiandaa kuuanza mwaka mpya, ni kupata muda wa kukaa na kutathmini nyendo zako na mambo yote yaliyotokea katika maisha yako kwa kipindi cha mwaka mzima.

Wengi huwa wanakumbuka kujadili mambo yao ya kimaisha ikiwemo kazi, malezi ya watoto, ujenzi wa nyumba, maendeleo ya biashara au vitu vinavyofanana na hivyo lakini huwa wanashindwa kufanya tathmini ya jambo muhimu zaidi; mapenzi na maisha ya ndoa.

Mipango yako yote inategemea amani ya moyo na utulivu wa akili yako, huwezi kuvipata vitu hivi kama utakuwa na migogoro ya mapenzi ndani ya ndoa au uhusiano wako kila kukicha.

Kwa kuzingatia hilo, ndiyo maana wataalam wa saikolojia ya mapenzi, wanashauri kwamba wakati ukikaa na kutafakari mafanikio na matatizo uliyokumbana nayo mwaka uliopita na kuandaa mikakati ya mwaka mpya, ni muhimu sana kulitazama suala la mapenzi kwa upana wake.

  1. ALIKUKOSEA NA WEWE UKAMKOSEA

Sisi si malaika, kila binadamu hukosea na hakuna mtu ambaye ni mkamilifu kwa asilimia 100. Yawezekana ukitafakari maisha uliyoishi na mwenzi wako kwa kipindi cha mwaka mzima uliopita, unayaona makosa makubwa aliyowahi kukufanyia.

Hiyo ni hatua ya kwanza lakini ya pili unapaswa kujitazama na wewe, lazima yapo ambayo ulimkosea na pengine kusababisha kulegalega kwa mapenzi yenu. Unapouanza mwaka mpya, ni muhimu sana kukaa na mwenzi wako na kwa pamoja mkajadili mambo mliyokoseana kwa lengo la kuyamaliza na kufungua ukurasa mpya.

Tafuta muda ambao nyote mtakuwa mmetulia, kila mmoja aeleze dukuduku lake na makosa aliyowahi kutendewa na mwenzake kisha kubalianeni kuweka pembeni tofauti zote za mwaka uliopita na kuangalia mwaka mpya.

  1. UMETIMIZA AHADI KWA KIWANGO GANI?

Lazima zipo ahadi ambazo ulimuahidi mwenzi wako, na yeye lazima zipo ahadi ambazo alikuahidi. Mnapoanza mwaka mpya, ni wakati wa kila mmoja kutathmini jinsi alivyotimiza ahadi alizomuahidi mwenzi wake.

Wahenga wanasema ahadi ni deni, hakuna kitu kibaya kama kumuahidi mwenzi wako jambo halafu ukashindwa kulitimiza bila kuwa na maelezo yoyote. Hebu orodhesha ahadi zote ambazo uliwahi kumpa na jiulize umezitimiza kwa kiwango gani?

Ukigundua ahadi nyingi zimekuwa hewa, ni wakati wa wewe kuzungumza na mwenzi wako kabla hata hajakukumbusha. Mueleze nini kilisababisha ukashindwa kutimiza ulichomuahidi, hiyo itamfanya aone kwamba wewe ni mtu unayejali, atauanza mwaka vizuri akiwa na uhakika kwamba yupo na mtu makini.

  1. UMEMSALITI MARA NGAPI?

Nilisema na nitaendelea kusema kwamba hakuna kitu kibaya kama usaliti. Wakati ukiuanza mwaka mpya, jiulize mwenyewe ndani ya moyo wako; ulimsaliti mwenzi wako mara ngapi? Yawezekana mwenyewe hajui lakini ndani ya moyo wako unao ukweli.

Kama hujawahi kumsaliti, una haki ya kujipongeza na kuendelea na moyo huohuo kwani uaminifu ndiyo nguzo kuu ya mapenzi. Hata hivyo, kama unajua kwamba umesaliti mara kadhaa, zungumza na moyo wako mwenyewe ni ahidi kwamba hutamsaliti tena na tekeleza ahadi hiyo kwa vitendo, bila kujali vishawishi unavyokutana navyo.

Tukutane wiki ijayo kwa mwendelezo wa mada hii. Kwa maoni, ushauri, nicheki kwa namba za hapo juu.

Comments are closed.