The House of Favourite Newspapers

Tumuombee Magufuli; anakabili mgogoro uliodumu miaka 50 Zanzibar

0

MAGUFULI ALIVYOAPISHWA LEO (62)TUMSHUKURU Mungu kwa kuwa tumempata rais mchapa kazi, Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliyeapishwa Alhamisi iliyopita jijini Dar es Salaam.

Lakini wakati tunafurahia tukio hilo, wengi hatuna furaha kutokana na rais huyo kubeba mgogoro mzito wa kisiasa visiwani  Zanzibar ambao umedumu kwa miaka 50 sasa tangu tuungane mwaka 1964.

Wazanzibari wamekuwa wakijaribu kupambana na madhara ya ajali ya kisiasa iliyoipata nchi yao ambayo imekuwa katika matatizo na muungano na chaguzi zao kwa miaka yote 50 ambapo sasa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 umefutwa.

Dk. Magufuli sijajua atatumia mbinu gani kumaliza tatizo hili zito la kuvurugwa kwa uchaguzi mkuu wa visiwani, lakini sote Watanzania tumuombee ili suala hilo liishe kwa amani.

Mbaya zaidi ni kwamba kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kulikotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha kumefanya baadhi ya Wazanzibar kuhusisha tukio hilo na muungano.

Zanzibar inakabiliwa na matatizo mengine mengi na tena makubwa sana. Hayo ni matatizo ambayo hata kama Zanzibar isingelikuwa kwenye muungano, bado yangelifanya libakie kuwa taifa lililo nyuma sana kimaendeleo ukilinganisha na mataifa mengine yaliyopata uhuru wakati Zanzibar ilipopata uhuru wake.

Kama kulivyo kwingine, hasa barani Afrika, Zanzibar pia kuna ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi wa serikali, kuna ugoigoi wa kijamii na utovu wa nidhamu wa umma lakini hayo yote Dk. Magufuli hawezi kuingilia kutokana na mipaka ya katiba ya nchi na huko visiwani wana katiba yao.

Hakuna ubishi kwamba ugoigoi wa kiutendaji umeonekana kwenye uchaguzi mkuu na kufanya kurudia uchaguzi jambo ambalo ni gharama na niseme wazi kwamba wale wote waliosababisha uchaguzi huu kufutwa nawaweka katika kundi la raia wasiotambua haki na wajibu wao kwa nchi, ambao wanaweza kuharibu mali ya umma au kutelekeza wajibu wao kwa kiwango cha juu.

 Zanzibar kuna mgogoro wa kisiasa ambao umedumu hata kabla Rais Magufuli hajawa waziri, miaka zaidi ya ishirini iliyopita, hivyo kukumbana na tatizo hilo, ni balaa.

Naamini wote waliohusika ‘kuumua’ tatizo hilo akilini mwao walijua kuwa kuna rais mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atapatikana baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, hivyo sijui kama walidhamiria kumtwisha mzigo huo Magufuli?

Hili ni tatizo kubwa la kikatiba linaloikabili Zanzibar na siyo jambo jepesi hata kidogo kwa kuwa linahusisha sheria mama inayoongoza nchi.

Hii ni ajali ya kisiasa. Ndiyo, ni ajali, tena mbaya. Ajali haisifiwi wala haikaribishwi. Ajali huweza kuepukwa lakini hii haikuepukwa.

 Bado Zanzibar haijawa na mageuzi makubwa yanayoonekana kuwa na matarajio kwa walio wengi na wengi wanalilia kuwe na serikali tatu kutokana na mambo kama hayo wanayofanya wachache.

Dk. Magufuli yupo madarakani, nirudie tena, nimuombee kwa Mungu na kumtakia kila la heri ili aweze kumaliza mgogoro huu wa Zanzibar kwa amani, awakutanishe Maalim Seif Sharif Hamadi wa CUF na Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM ili ufumbuzi upatikane. Tumuombee amalize mgogoro huu uliodumu kwa miaka zaidi ya 50!

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply