The House of Favourite Newspapers

Tumuombeeni Mzee Majuto!

0

Stori: Brighton Masalu | IJUMAA WIKIENDA

DAR ES SALAAM: Tumuombeeni! Lejendari wa vichekesho Bongo, Amri Athman ‘Mzee Majuto’ yu taaban kwa takriban wiki mbili sasa kufuatia kubanwa na ugonjwa wa ngiri huku mkewe, Mama Bilal naye akisumbuliwa na homa, jambo ambalo staa huyo ameomba Watanzania wamuombee.

KUTOKA TANGA

Katika mazungumzo na Wikienda kwa njia ya simu akiwa nyumbani kwake, Tanga, Mzee Majuto alisema kuwa, ni wiki ya pili sasa hali yake kiafya si nzuri, mara nyingi amekuwa akitumia dawa za hospitali na zile za kienyeji lakini hakuna unafuu wowote anaoupata.

“Nasumbuliwa sana na ngiri, sasa nakwenda wiki ya pili na siku kadhaa, hali si nzuri kabisa na kuna kipindi nililazwa, lakini sikupata nafuu, dawa nimemeza hadi nahisi nina stoo ya madawa tumboni, mama Bilal (mkewe) ambaye ndiye msaidizi na mhudumu wangu, naye anasumbuliwa na homa kali, namlilia Mungu juu ya jambo hili,” alisema Mzee Majuto.

NGIRI NI UGONJWA GANI?

Katika kujiridhisha kwa undani zaidi juu ya ugonjwa huo, Wikienda lilizungumza na baadhi ya madaktari bingwa ambao kwa nyakati tofauti walitoa ufafanuzi toshelezi juu ya tatizo hilo linalosumbua watu wengi.

“Ngiri au hernia ni aina ya ugonjwa ambao unampata mtu baada ya misuli au kuta za tishu mwilini zinazoshikilia au kubeba viungo (organs) fulani kupoteza uimara au kuwa na uwazi (opening) hivyo kusababisha viungo hivyo kutoshikiliwa ipasavyo,” alisema mmoja wa madaktari walioulizwa na Wikienda na kuongeza:

“Tatizo la ngiri huweza kumpata mtu yeyote. Miongoni mwa vitu vinavyoweza kumsababisha mtu apate ugonjwa wa ngiri ni kuwa na uzito mkubwa au kuongezeka uzito kwa ghafla, kazi ya kubeba au kunyanyua vitu vizito, tatizo la kukohoa au kupiga chafya kwa muda mrefu, ujauzito au matatizo yanayojitokeza kwa mwanamke wakati wa kujifungua. Pia kuharisha au kuvimbiwa (constipation). Vitu hivyo humfanya mtu apate ngiri (hernia).

Mze Majuto akiwa na familia yake.

“Ngiri hutambuliwa kwa kutokea kitu kama uvimbe au kujaa katika eneo husika (baadhi ya maeneo yametajwa hapo juu) na pia kwa kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara na daktari huwezesha kugundua tatizo hili.

“Njia inayoweza kutatua tatizo hilo ni kwa mtu mwenye ngiri kufanyiwa upasuaji ili kurekebisha misuli au tishu zilizolegea.

“Pia kutegemeana na kihatarishi cha tatizo hili, mtu unaweza kuwa unafanya mazoezi ili kupunguza uzito wako na kuweka utaratibu mzuri wa kula chakula kinachojumuisha mbogamboga au matunda yenye nyuzi (fibers). Hii itasaidia pia mmeng’enyo (digestion) wa chakula tumboni na kuepusha kuvimbiwa.

“Matunda (Vitamin C) husaidia kuunganisha tishu zilizolegea na pia husaidia kupona haraka kwa sehemu iliyofanyiwa upasuaji. Na kama tatizo lako ni la kukohoa kwa muda mrefu kunakosababishwa na uvutaji wa sigara, ni vyema ukasitisha uvutaji ili kupunguza madhara au makali ya ngiri, lakini pia kusitisha sigara kwa ajili ya usalama wa afya yako.”

Naye Dk Annelie Mpasu, mtaalam wa magonjwa sugu ya binadamu, alisema: “Sehemu inayoathiriwa mara nyingi ni maeneo ya tumbo, kokwa, korodani na kadhalika ambapo baadhi ya viungo vya mwili vilivyomo tumboni hujipenyeza kupitia vitundu vinavyopitisha mishipa ya fahamu inayohudumia kokwa (spesmatic cord), hivyo baada ya kujipenyeza huteremka hadi ndani ya korodani hali ambayo hukamilisha kuwepo kwa ugonjwa wa mshipa wa ngiri.

“Maeneo sugu ambayo ngiri hutokea ni pamoja na tumboni, eneo la juu ya paja, kifuani na eneo ambalo mtu aliwahi kufanyiwa upasuaji.”

AINA ZA NGIRI

Kwa mujibu wa duru za kiafya, zipo aina tofauti za ugonjwa huo ambazo ni kama zifuatazo;

Ngiri-maji –Hii ni aina ya ngiri ijulikanayo pia kwa kitaalam kama (hydrocele).

Ngiri-kavu (hernia) – hujulikana pia kama ‘fermoral hernia’ kwa wanawake na huitwa ‘scrotal hernia’ kwa wanaume.

Ngiri ya kwenye kifua – hujulikana pia kitaalam kama ‘hiatus hernia’.

Ngiri ya tumbo –hujulikana pia kama ‘abdominal hernia’.

Ngiri ya kwenye kitovu – hujulikana pia kama ‘umbilical hernia’.

Ngiri ya sehemu ya haja kubwa – hujulikana pia kama ‘anal hernia’.

Hata hivyo, dalili za aina zote za ngiri hazitofautiani na ngiri hujitokeza bila maumivu yoyote ingawa kuna baadhi ya ngiri huwa na maumivu makali kutegemeana na ngiri ilivyotokeza.

Leave A Reply