The House of Favourite Newspapers

Tunaadhimisha mashujaa, je tunawakumbuka?

0

OTH_9308Kwanza nimshukuru Mungu kwa kunipa uhai na afya tele na kuniwezesha kuandika haya leo.

Leo nizungumzie sikukuu ya mashujaa ambayo huadhimishwa Julai 25, kila mwaka nchini.

Mashujaa katika nchi hii wapo wengi, wengine waliifia nchi yetu nje ya nchi, wengine ndani kwa kupigania ardhi yetu.

Tunajua wakati wa kupigania uhuru wa nchi mbalimbali barani Afrika, wanajeshi wetu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walishiriki kung’oa serikali mbalimbali za kikoloni.

Baadhi ya wapiganaji hao wapo hai na wengi wao wamestaafu. Je, tunawakumbuka? Au wamebaki majumbani wakitaabika? Katika nchi zilizoendelea wastaafu kama hao hupewa heshima ya kipekee.

Kwa mfano, wenzetu kama Wamarekani wanajeshi wao waliopigana vita kwa ajili ya nchi yao wanapewa vitambulisho maalum ambavyo vinawawezesha kupanda mabasi ya umma au maduka maalum na kupunguziwa bei.

Jambo hilo unaweza kuona kuwa ni kitu kidogo lakini ukweli ni kwamba linatoa faraja kwa watu hao waliokuwa tayari kutoa uhai wao kwa ajili ya kupigania nchi yao.

Hata humo ndani ya chama tawala, kuna baadhi ya waasisi wa chama walipigania uhuru lakini leo hii wapo katika hali mbaya sana ya kimaisha. Je, hakuna njia ya kupunguza makali ya maisha yao.

Nikisema niwataje wote waliopigania nchi hii kwa udi na uvumba naweza kujaza nafasi hii, lakini ndani ya jamii na hata serikalini wanafahamika.

Sidhani kama ni gharama kubwa kuwaangalia mashujaa hao kwa sababu kadiri siku zinavyosonga, ndivyo wanavyozidi kupungua kwa sababu mbalimbali.

Nimekuwa nikifuatilia siku ya mashujaa kwa hapa kwetu Tanzania kwa miaka tele. Kwa hapa kwetu  siku ya mashujaa hukumbukwa wale tu waliopigana vita na kufariki dunia.

Hapo juu nimetoa mfano wa Marekani jinsi wanavyowaenzi watu waliopigania taifa lao na kwa Kenya imekuwa tofauti kidogo kwani wao shujaa wanamtambua kwa mapana zaidi. Hata yule mwana michezo aliyeliletea sifa taifa basi naye pia ni shujaa anayeenziwa.

Nchini Kenya shujaa ni mtu aliyeliletea taifa mafanikio katika nyanja mbalimbali. Hongera Kenya kwa kutambua michango ya raia wenu katika taifa.

Ipo haja ile kamati ya maadhimisho nchini kuangalia wazo hili nililolitoa kwa sababu kuwaenzi waliokuwa tayari kutoa uhai wao kwa ajili ya nchi ni njia mojawapo ya kuhamasisha uzalendo ambao sasa kila mtu ni shahidi kwamba umekufa ndiyo maana tumezalisha mafisadi, neno ambalo tulikuwa tunalisoma tu katika vitabu vya zamani au kulisikia nchi jirani.

Naamini, tukianza kuwaenzi mashujaa wa nchi hii, pamoja na wale ambao wapo hai, basi tutachochea uzalendo na kila mtu atakuwa anajua kuwa kumbe ukiwa mzalendo unaenziwa na taifa. Sipingi kuwaenzi wale waliofariki dunia, lakini walio hai nao wakumbukwe.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply