The House of Favourite Newspapers

Tunachojifunza Mauaji ya Kimbari Rwanda-3

Watanzania wengi hawajui nini kilisababisha mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda yaliyosababisha mamia ya watu kuuawa kikatili sana. Naamini kama wakisoma makala haya watajifunza kitu na kuona umuhimu wa mshikamano na amani tulionao na faida yake. Endelea…

WIKI iliyopita tulikuwa tunaelezea kuhusu jumba la makumbusho lililopo Kigali, Rwanda lililobeba historia ya kutisha ya mauaji ya kinyama ya kimbari. Kwa nje ya makumbusho hayo kuna makaburi makubwa walimozikwa mamia ya watu. Lipo kaburi la wazi la kioo.

Inaelezwa kwamba baada ya machafuko ya vita ikawa mamia ya mafuvu ya binadamu yaligunduliwa sehemu mbalimbali hivyo kuchukuliwa na kuja kuzikwa pale kiheshima.

Ni vema kuangalia historia ya Rwanda kabla ya mauaji haya au kabla ya ukoloni. Inaelezwa

watu wa kwanza kuishi katika eneo ambalo leo tunalitambua kama nchi ya Rwanda ni watu wa kabila la ‘Twa’ (Watwa).

Kabila hili la wawindaji si la kibantu bali ni sehemu ya makabila yanayotambulika na wanahistoria kama ‘pygmy’ ambao sifa yao kuu ni ufupi. Watwa waliishi Rwanda enzi za kale sana miaka ya 8000 BC na 3000 BC.

Kuanzia miaka ya 700 BC mpaka 1500 AD makabila ya Kibantu kutoka maeneo ya jirani yalianza kuhamia eneo hili.

Kuna nadharia mbalimbali kuhusu ni namna gani haswa makabila haya ya kibantu yalihamia hapa na baadaye kusababisha kutokea makabila ya sasa ya Wahutu na Watusi.

Nadharia ya kwanza inadai kwamba; Wahutu ndio walikuwa wa kwanza kuhamia eneo hili na kuanzisha shughuli za kilimo. Baadaye watu wenye asili ya Ukushi (Watusi wa sasa) nao wakahamia kwenye eneo hili na kulitawala.

Nadharia ya pili inadai kwamba, kuna uwezekano Watusi si Wakushi bali ni wahamiaji tu kutoka maeneo ya jirani kipindi hicho cha kale ambao walihamia na kujichanganya na jamii waliyoikuta hapo (Wahutu) lakini wao walikuwa wafugaji.

Chini ya nadharia hii inadaiwa kwamba kuibuka kwa Wahutu na Watusi hakukutokana na kuwa na utofauti wa kinasaba au asili ya mababu bali ulitokana na utofauti wa kimadaraja/ matabaka ya kijamii.

Tabaka la wale walio wa daraja la juu ambao walikuwa wafugaji walijitanabahisha kama Watusi wakati ambapo tabaka la chini ambao walikuwa wakulima walijitanabahisha kama Wahutu.

Makabila haya yote matatu, Watwa, Wahutu na Watusi wanazungumza lugha moja na kwa wote kwa pamoja wanajulikana kama Banyarwanda.

Idadi ya watu ilipoongezeka katika eneo hili walianza kujitambua kupitia makundi madogomadogo yaliyoitwa ‘Ubwoko’ au ‘koo’ kwa Kiswahili. Ilipofika katikati ya miaka ya 1700 koo nyingi ziliungana na kuunda falme.

Moja ya falme ambazo zilikuwa imara zaidi ulikuwa ni ‘Kingdom of Rwanda’ ambayo watawala wake wote walitokea katika koo ya Kitusi ya Nyiginya.

Ufalme huu ulifikia kileleni kipindi cha utawala wa Mfalme Kigeli Rwabugiri chini ya falsafa yake ya kujipanua na kuteka falme nyingine na kuzifanya sehemu ya Kingdom of Rwanda.

Chini ya Mfalme Rwabugiri alianzisha mfumo wa kiuchumi wa ‘ubuhake’ na baadaye ‘uburetwa’.

Katika mifumo yote hii miwili, iliwanufaisha zaidi Watusi na kuwafanya Wahutu kama vijakazi wao wa kuwafanyia kazi za uzalishaji na kuwa askari vitani kwa ujira wa kupata fursa ya kumiliki mifugo na kutumia ardhi.

Watusi walipaa juu zaidi na kuwa raia daraja la kwanza na Wahutu kubakia kuwa tabaka la chini kabisa ndani ya Kingdom of Rwanda.

Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 ulilitoa eneo hili la Rwanda kuwa koloni la nchi ya Ujerumani. Wajerumani walitawala eneo hili kwa kushirikiana na mfalme na hivyo kuwapa wepesi wa kutawala koloni bila kuwa na askari wengi wa Kijerumani ndani ya ardhi ya Rwanda. Yuhi V Musinga ndiye alikuwa Mfalme wa Rwanda kwa kipindi hicho na anakumbukwa zaidi kwa kuwapokea Wajerumani kwa mikono miwili.

Wajerumani ndio walikuwa watu wa kwanza kuanza kuwapandikizia Watusi kasumba ya kuwa wao si Wabantu.

Wakoloni wa Ujerumani ndio ambao walieneza propaganda kwa kuwafundisha Watusi kwamba kutokana na tafiti zao za kina wamegundua wao (Watusi) mababu zao wa kale walihamia eneo hilo kutokea Ethiopia.

Hivyo wakawashawishi kuamini kwamba Watusi wana vinasaba vya ‘uzungu’ (Caucasian) na hivyo ni wao pekee ndani ya Rwanda walistahili kupata nafasi za ajira chini ya utawala huo wa Wajerumani.

Nini kilifuata? Fuatilia hapahapa Jumanne ijayo.

Comments are closed.