The House of Favourite Newspapers

Tunachojifunza Mauaji ya Kimbari Rwanda -4

Watanzania wengi hawajui nini kilisababisha mauaji ya kimbari ya nchini Rwanda yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa kikatili. Naamini kama wakisoma makala haya watajifunza kitu na kuona umuhimu wa mshikamano na amani tulionao na faida yake.

SASA ENDELEA…

WIKI iliyopita tulisoma jinsi mama mmoja alivyoponea tundu la sindano baada ya kupigwa na kukatwa mkono na kulazimishwa kunywa damu za maiti siku ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda mwaka 1994.

 

Mama huyo alioneshwa ‘laivu’ kwenye hafla ya kumbukumbu ya mauaji hayo ya Rwanda iliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar, Jumamosi ya Aprili 7, mwaka huu na mgeni rasmi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harisson Mwakyembe.

Leo nilidhani ni vema nikaanza kueleza historia ya nchi hii na makabila ya Wahutu na Watusi ya Rwanda.

 

Niliwahi kusema kwamba Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884 ulilitoa eneo hili kuwa koloni la nchi ya Ujerumani. Wajerumani walitawala eneo hili kwa kushirikiana na mfalme na hivyo kuwapa wepesi wa kutawala koloni bila kuwa na askari wengi wa Kijerumani ndani ya ardhi ya Rwanda. Yuhi V Musinga ndiye alikuwa Mfalme wa Rwanda kwa kipindi hicho na anakumbukwa zaidi kwa kuwapokea Wajerumani kwa mikono miwili.

Wajerumani ndiyo walikuwa watu wa kwanza kuanza kuwapandikizia Watusi kasumba ya kuwa wao si Wabantu.

 

Katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia ya 1917- 1919, Ubelgiji iliziteka Rwanda na Burundi kutoka mikononi mwa Ujerumani na mwaka 1919 Umoja wa Mataifa ilizifanya rasmi nchi hizo kuwa makoloni ya Ubelgiji.

Mwanzoni wakoloni wa Ubelgiji walianza kuitawala Rwanda kwa mtindo uleule wa kushirikiana na ‘ufalme’ lakini baadaye wakajilimbikizia madaraka yote ya kutawala kama ambavyo walifanya kwenye koloni lao la Kongo.

 

Baadaye wakaanza ‘kutaifisha’ mali za Wanyarwanda katika mfumo wa kufanana kabisa na mfumo wa asili na walioathirika zaidi na kampeni hii ya utaifishaji walikuwa ni Wahutu.

Ardhi yao ilinyang’anywa, mifugo ilichukuliwa na kuwafanya Wahutu kuwa si tu vijakazi wa wakoloni, bali pia vijakazi wa Watusi.

 

Mwanzoni mwa miaka ya 1930, Ubelgiji walifanya upanuzi mkubwa wa sekta ya elimu, afya na ajira za umma. Lakini wanufaika wakuu walikuwa ni Watusi.

Mwaka 1935, Ubelgiji walifanya kitu cha ajabu sana ambacho kilipanua zaidi mpasuko wa kijamii na kitabaka uliopo ndani ya Rwanda. Walianzisha mfumo wa raia wote kuwa na vitambulisho. Vitambulisho hivi viliwatambua raia wote katika makundi manne kulingana na makabila yao. Watwa, Wahutu, Watusi na Raia wa kuomba (Naturalised).

 

Kutokana na Watusi kuwa ndiyo raia wa daraja la kwanza na tabaka la juu huku Wahutu wakiwa ni watu hafifu wa kudharaulika nchini humo, ilifikia hatua Wahutu wenye mali au ushawishi walikuwa wanahonga fedha ili kupatiwa vitambulisho vya kuonesha ni Watusi na watawala hawakuwapa Utusi kamili bali waliwapa ‘utusi wa heshima’ (Honorary Tutsi), ubaguzi mbaya sana huu ambao Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa akipinga.

Hadhi ya Wahutu wote iliendelea kushuka kwa kasi wakionekana ni kabila na kizazi cha wasioelimika huku Watusi wakionekana ndicho kizazi cha ‘wastaarabu’ na kabila lenye daraja A.

 

Lakini kuna suala ambalo lilifanyika mwanzoni likionekana kuwa na manufaa makubwa, lakini kadiri siku zilivyokwenda lilianza kuwa kama mkuki mgongoni.

Kanisa Katoliki lilikuwa limeenea sana nchini Rwanda na raia wake wengi wakiwa ni waumini wa kanisa hilo. Tukumbuke kwamba tangu kipindi hicho Wahutu ndiyo walikuwa idadi kubwa zaidi ya raia wote ndani ya Rwanda. Hii ilimaanisha pia kwamba waumini wengi wa Kanisa Katoliki walikuwa ni Wahutu.

 

Kwa kiasi fulani ndani ya Kanisa Katoliki mapadri na watawa wengine walikuwa wanajisikia hatia kuacha waumini wao kuwekwa kwenye kundi la kizazi cha ‘wasiostaarabika’ na kudharaulika ndani ya jamii. Kwa hiyo zikaanza juhudi za makusudi za Kanisa Katoliki kutoa elimu kwa vijana wenye asili ya Kihutu.

 

Baada ya miaka kadhaa kukaanza kuwepo walau kidogo uwiano wa wasomi wa Kihutu na Kitusi.

Mwaka 1957, mwezi Machi kikundi cha wasomi na watu wenye ushawishi wenye asili ya Kihutu walifanya jambo la ‘kimapinduzi’ ambalo lilipanda mbegu mpya kwenye nafsi za watu wa kabila na kizazi cha cha Kihutu.

 

Waliandaa waraka ulioitwa ‘Manifeste Des Bahutu’ (Bahutu Manifesto).

Huu ndiyo ulikuwa waraka wa kwanza rasmi kubainisha kwamba Wahutu na Watusi ni makabila mawili (race) tofauti.

Je, nini kilifuata? Fuatilia hapahapa Jumanne ijayo.

Comments are closed.