The House of Favourite Newspapers

Tundu Lissu atarejea, hatarejea nchini?

TAKRIBAN mwaka mmoja na ushee sasa Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu yupo nje ya nchi. Alianza kuwa Nairobi nchini Kenya na baadaye kwenye kampasi ya Chuo cha Gasthuisberg, Leuven nchini Ubelgiji kwa ajili ya matibabu.

Hivi sasa Lissu ametoka hospitali na amefanya ziara katika nchi za Ulaya na sasa yupo Marekani na amezua minong’ono na tetesi kuwa je, atarudi nchini au hatarudi nchini?

Mara tu matibabu yake Lissu yalipohamishiwa Ubelgiji, zilienezwa taarifa zisemazo kuwa anaweza kuhamia huko moja kwa moja. Tetesi zikawa nyingi, hasa baada ya hivi karibuni kutoa matamko makali dhidi ya Serikali. Wapo waliosema ataishi Ujerumani. Wengine wakasema Sweden na sasa imeongezwa nchi ya Canada.

Tetesi za kuhama nchi zimekuwa ni mjadala kila anapozungumza na wana habari huko nje ya nchi kwani huulizwa na wanahabari na yeye kuwahakikishia kuwa atarudi kuishi nchini kama ataambiwa na madaktari wake huko Ubelgiji kuwa sasa amepona.

Kusisitiza kwamba atarudi nchini, Lissu amekuwa akisema waziwazi ugumu wa kuwa nje ya nchi kimatibabu na kutokuonana moja kwa moja na watu mbalimbali aliozoea nao hapa nyumbani wakiwemo ndugu, jamaa, majirani na marafiki.

Lakini amekuwa akisema jinsi anavyokerwa kufuatilia mapambano ya kudai haki na demokrasia mitandaoni badala ya kuwa mshiriki kwenye ‘uwanja wa mapambano’ hapa nyumbani hasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambapo mwaka huu 2019 wana uchaguzi kuanzia ngazi ya chini hadi ya mwenyekiti wa taifa, nafasi inayoshikiliwa na Freeman Mbowe.

Lissu amekuwa akidai haki ya kugharamiwa matibabu akielezea haki ya mbunge kutibiwa kwa gharama ya kodi ya wananchi, ni kweli sheria ya uendeshaji wa Bunge, 2008, inasema kuwa kila mbunge atakuwa na haki ya kutibiwa ndani au nje ya Tanzania kwa gharama ya Bunge, lakini kila jambo lina utaratibu wake.

Pengine Bunge haliwajibiki kulipa gharama za matibabu ya Lissu kama anavyoeleza Spika Job Ndugai kwa sababu alikiuka au viongozi wa chama chake bungeni walikiuka taratibu za matibabu ya wabunge kwa kulazimisha kupelekwa Nairobi badala ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwanza, hili nalo lina uzito wake.

Hospitali ya Muhimbili kupitia madaktari bingwa kwa mujibu wa Spika Ndugai ilitakiwa watoe mapendekezo ya Lissu kupelekwa nje kutibiwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ambaye naye angeunda jopo la madaktari watatu kuchunguza mapendekezo ya Muhimbili.

Kama ilivyo ada katika hili Lissu analalamika kwa kusema majeraha aliyokuwa nayo na kwa hali ya kiusalama iliyokuwepo, hakukuwa na uhakika kwamba akipelekwa Muhimbili atakuwa salama dhidi ya watu waliomshambulia.

Hivyo Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe wakajichukulia uamuzi wao wa kumtia matatizoni kwa kumpeleka Nairobi, Kenya badala ya Hospitali ya Muhimbili.

Viongozi wa Chadema wanasema kuwa hakukuwa na muda mrefu wa kusubiri hali itulie hivyo hawakutaka kufuata taratibu za kibunge za kumhudumia mbunge, wakaamua walivyoamua, najiuliza hizo taratibu ambazo Spika Ndugai anazisema mara kwa mara akina Mbowe walizijua?

Jambo linalotolewa mfano ni la Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangallah baada ya kupata ajali mbaya alichukuliwa na helikopta na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tofauti na Lissu ambaye viongozi wake walivunja utaratibu na kumpeleka Kenya kisha Ulaya.

Kuhusu madai ya Lissu kwamba vyombo vya dola havishughulikii upigwaji wake risasi, wapinzani wake kila kona ya nchi wanahoji kwa nini hadi leo bado amemzuia dereva wake kurejea nchini ili ahojiwe na Polisi? Wanasema yeye ni shahidi muhimu katika shauri lake.

Watu wanasema Lissu ana kipaji, lakini kitumike kwa uzalendo kwa nchi yake na si kipaji chake cha kuongea akitumie kuchafua nchi yake huko Ulaya na Marekani mbele ya Wazungu wasiotutakia mema.
Lakini swali la wapinzani wake linakuwa kwa nini Lissu ameamua kutembelea nchi za Ulaya na Marekani huku akitaja mambo mazito na kuihusisha Serikali? Hapo ndipo minong’ono kwamba hatarudi nchini inapopamba moto licha ya yeye na viongozi wa Chadema kukanusha.

Wanasema kwa nini Lissu asitumie nafasi hiyo Ulaya na Marekani kuomba misaada kwa wananchi wa jimbo lake la Singida Mashariki akiwaeleza Wazungu kwamba msemaji wao ambaye ni yeye, yupo nje ya jimbo kwa zaidi ya mwaka sasa, hivyo watu wake wanahitaji misaada ya kijamii kama vile visima, shule na kadhalika?

Wakati Lissu akidai kwamba Serikali haifanyi chochote cha maana, wapinzani wake wanafurahia ujio wa ndege za Airbus na Dreamliner, ujenzi wa reli mpya ya Standard Gauge, ujenzi wa bwawa kubwa la kuzalisha umeme la Stigglers Gorge na Flyover za kwanza Tanzania.
Hizo ndizo siasa za siasa, naomba kutoa hoja!

Siasa za Siasa

Na Elvan Stambuli

Simu: 0674- 339616

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.