The House of Favourite Newspapers

TUOMBE WEMA SEPETU APATE MTOTO; LAKINI…..

Wema Sepetu

EEE Mungu naomba mtoto na mimi. Andika ameeni!  Haya ni maneno niliyoyatoa kwenye Mtandao wa Facebook katika Ukurasa wenye jina la Team Wema Sepetu Tz. Lengo la ujumbe huo ulioambana na picha ya Miss Tanzania 2006, Wema ni kuwahamasisha marafiki zake wamuombee dua, jicho la Mungu limuone naye aweze kupata mtoto.

Yawezekana kabisa Wema hakulituma kundi wala mtu yeyote kumuombea apate mtoto; lakini hakuna ubishi kwamba, walio nyuma yake wanatamani apate uzao. Binafsi nilifuatilia sana hamasa hiyo iliyoshika kasi wiki iliyopita, nikajipa muda wa kutosha kusoma komenti za rafiki wa Wema katika posti nyingi za aina hiyo, nikajifunza kitu kwamba:

 

“Watu wanaweza kukupenda lakini wewe usijipende.” Kwanza nimuombe radhi Wema kwa sababu hiki ninachotaka kukizungumzia kinatoka mikononi mwa Mungu, nami sikusudii kupingana na mapenzi ya Mungu. Lakini hoja yangu itakuwa kwenye hiyo hamasa ya Team Wema ya kumuombea miss huyo apate mtoto; cha kwanza kujiuliza ni kweli kwamba anahitaji mtoto? Kwa kuwa swali hili alishalijibu mara kadhaa kwamba, anahitaji  sana kuitwa mama; tumuulize jingine:

 

“Kwa nini hakai kwenye foleni ya watafuta mtoto kama kweli ni mhitaji?”

Tuache mambo ya kitoto ya kuulizana ni foleni ipi alitakiwa kupanga? Sote tunajua namna ambavyo mtoto hupatikana hasa kwa mapenzi ya Mungu ambaye Team Wema wanamuomba heri yake. Kushirikisha watu kumumbea mtu asiyekuwa na mume azae, hiki nacho ni kituko cha aina yake; anazaaje kwa mfano?

Kama kweli Wema na wafuasi wake wamekusudia kabisa kupeleka maombi kwa Mungu ili mtoto apatikane hilo ni jambo jema lakini wangeanza kumuombea Wema apate mume halafu ndipo suala la mtoto lifuate. Wema naye atafute mume kwanza kabla ya kutafuta mtoto, ama sivyo Wema atuambie kuwa   yeye ni muumini wa ‘Bahati Mbaya’ na kwamba anataka kupata mtoto kwa bahati mbaya kwa kukutana kimapenzi kibahati mbaya.

 

Ngoja nimpe Wema na wafuasi wake kisa hiki: Nchini Uingereza mwanamke aitwaye Naomi Gryn alipata mtoto wake wa kwanza akiwa na umri wa miaka 51 baada ya kuhangaika kwa muda mrefu. Akiwa katika umri sahihi wa kupata mtoto ambao ni kati ya miaka 20-35 Naomi anasema alikuwa kiruka na kila mwanaume aliyekwea mbawa zake. Uzuri ulimsukuma kufanya atakavyo kwa kila mwaume. Kipindi hicho hakuona umuhimu wa kuwa na mtoto ilikuwa ni kuponda raha kwa kwenda mbele.

 

Kiu ya Naomi kuwa na mtoto ilikolea alipofika miaka 40. Hata hivyo, alipokuwa katika kujutia zoazoa yake alikutana na mwanaume mmoja aitwaye Peter ambaye alikuwa amemzidi miaka minane, hapo ndipo alipoamua kukaa katika foleni ya watafuta mtoto akiwa na mwanaume huyo. Lakini akiwa mwenye matumaini ya kuzaa akapata ajali iliyomsababishia majeruhi yaliyomuweka kando ya wazo lake la kupata ujauzito kwa miaka mingi.

 

Wakati akitafuta afya, umri ulikuwa unazidi kumtupa mkono, madaktari wa masuala ya uzazi walizidi kumtisha pale walipompa takwimu kuwa wanawake wenye umri mkubwa suala la kuzaa ni hatari zaidi kwao. Hata hivyo, hakukata tamaa, aliendelea kukaa kwenye foleni akiwa na mpenzi wake huyo mmoja, Peter, Walivumiliana kwa kila hali, walitafuta tiba kwenye kliniki nyingi za masuala ya uzazi huku wakiomba Mungu awajalie wapate mtoto.

 

Naomi anasema alipoanza kusikia dalili za ujauzito alizokuwa akisimuliwa hakuamini hadi alipokwenda hospitali kupima ambako aliambia kuwa ana ujauzito kwa asilimia mia, jambo lililomfanya arukeruke kwa furaha. Naomi amezaa mtoto wake wa kwanza akiwa na miaka 51 kama nilivyosema, hakuamini na leo amekuwa mfano wa warembo wengine.

Kisa hiki kinafanana kwa namna fulani na maisha ya Wema, miss huyu amekuwa mrembo anayeamini kuwa naweza kuruka na mwanaume amtakaye bila kikwazo, kapita kwingi kila mtu anafahamu. Mfanano mwingine wa Wema na Naomi ni kwamba wakati anahangaika kupata ujauzito kuna suala la kufanyiwa upasuaji katika tumbo lake la uzazi lilimkuta Wema hivi karibuni kama vile Naomi alivyopata ajali.

 

Pengine kilichosalia kuwafananisha kabisa ni Wema kuamua kuwa na mtu mmoja atakayemuweka kwenye foleni ya uzazi ili hata kama umri utaonekana kumtupa mkono maombi ya Team Wema naamini yanaweza kumsadia akapata mtoto wa kumfariji. Ni vyema Wema akafahamu kwamba suala uzazi liko kibaiolojia, kisaikolojia na kiimani mambo haya yote yanayotegemeana.

 

Ikumbukwe kuwa suala la kibaiolojia linaposhindwa kuleta matokeo ya haraka, huzaa tatizo la kisaikolojia la watu kukucheka, kujiona mwenyewe hufai na hali ya kukata tamaa, hapo ndipo Mungu huweza kushirikishwa ili asaidie mahali ambapo mkono wa binadamu umeshindwa kufika. Naamini si Wema tu hata na wasichana wengine wanaohangaika kupata watoto wanayo nafasi ya kuzaa endapo watakaa kwenye foleni ya uzazi kwa kufuatilia afya zao, kuwa na waume sahihi na kumtumaini Mungu kwa kila jambo.

 

Vinginevyo kutafuta mtoto kwa njia za bahati mbaya, za leo umelala na huyu kesho yule na keshokutwa mwingine utajikuta umezeeka. Namalizia kwa kusema hivi; ninyi Team Wema, kumuombea Wema azae ni sawa lakini aombewe kwanza apate mume, hayo mengine ya mbona fulani kazaa kabla hajapata mume tuyaache mikononi mwa Mungu.

MAKALA: Mwandishi Wetu.

Comments are closed.