The House of Favourite Newspapers

TUTAKAMILISHA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MUSOMA -MAJALIWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Gaudencia Kabaka baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Musoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya wananchi waliofika kwenye uwanja wa ndege wa Musoma  kumlaki baada ya kuwasili  mjini Musoma kuanza ziara ya Mkoa  wa Mara. 
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifurahia ngoma ya Rirandi  ya asili ya kabila la Wakurya baada ya kuwasili  kwenye uwanja wa ndege wa Musoma.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua  majengo ya Shule ya  Secondari ya Ufundi Musoma ambapo serikali imetoa shillingi bilioni 1.28 kwa ajilli ya ukarabati huo.  Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na kulia kwake ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Mara, Samweli Kiboyi. Kushoto ni Mkuu wa Shule hiyo, Mutta Venance.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akitoka ndani ya bweni la Shaban Robert wakati  alipokagua ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Musoma.
Majliwa akikagua ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara ya  Mwalimu Nyerere iliyopo Kwangwa mjini Musoma.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amsema Serikali itahakikisha inakamilisha ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Mara iliyoanza kujengwa mwaka 1980.

 

Atoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 15, 2018) wakati alipokagua ujenzi wa hospitali hiyo baada ya kuwasili mkoani Mara kwa ajili ya ziara yake ya kikazi.

 

Waziri Mkuu amesema Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa awamu, ambapo wataanza na eneo la mapokezi na vyumba vya madaktari.

 

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha huduma za afya nchini, hivyo amewaomba wananchi waendelee kuiamini na kushirikiana nayo.

Waziri Mkuu amesema tayari Serikali imetoa sh. bilioni 1.4 ili ujenzi uendelee. Ujenzi huo ulianza mwaka 1980, ulisimama mwaka 1987 kuanza tena 2010.

 

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekagua uwanja wa ndege wa Musoma mkoani Mara ambao unatarajiwa kukarabatiwa na kuwekwa lami.

 

Amesema kukamilika kwa ukarabati huo wa kiwanja hicho kutafungua fursa za utalii ndani ya mkoa huo ambao umezungukwa na vivutio vingi.

 

Amesema Serikali imedhamilria kukarabati viwanja mbalimbali vya ndege nchini kikiwemo cha Musoma ili kuboresha huduma za usafiri wa anga.

 

Viwanja vingine vinavyotarajiwa kukarabatiwa ni Iringa, Kilwa Masoko, Lake Manyara, Lindi, Moshi, Njombe, Tanga, Simiyu, Singida na Songea.

 

Waziri Mkuu amesema viwanja hivyo kwa sasa vinakarabatiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), ambao wanajenga kwa gharama nafuu na kwa viwango vinavyostahili.

 

Awali, Meneja wa TANROADS, mkoa wa Mara Mhandisi Mlima Ngaila alisema ukarabati huo utafanyika kwa awamu tatu ambapo ya kwanza itahusisha upanuzi wa uwanja na ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege.

 

Alisema barabara ya kuruka na kutua ndege ina urefu wa km. 1.6 na upana wa mita 33 ni ya changarawe, hivyo kusababisha baadhi ya ndege kushindwa kutua.

 

Pia, Waziri Mkuu alikagua ukarabati wa Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Musoma na kwamba ameridhishwa na ukarabati wa miundombinu ya shule hiyo.

 

“Shule hii ilipewa sh bilioni 1.28 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu. Nimekagua jengo la utawala, madarasa, mabweni, jiko, maabara na bwalo, nimeridhika na kazi iliyofanyika.”

 

Shule hiyo ni miongoni mwa shule 10 kongwe ambazo Serikali iliamua kuzikarabati ili ziweze kurudi kama zamani na kuendelea kutumika.

 

Hata hivyo Waziri Mkuu aliuagiza uongozi wa Manispaa ya Musoma kushirikiana na uongozi wa shule hiyo katika kutatua baadhi ya changamoto zinazoikabili.

 

Miongoni mwa changamoto hizo ni malipo ya watumishi wasaidizi wakiwemo wapishi, walinzi na madereva, ambapo aliitaka kuchukua jukumu la kuwalipa watumishi hao badala ya kuacha jukumu hilo kwa Mkuu wa Shule.

Comments are closed.