The House of Favourite Newspapers

Tuyisenge kimeeleweka Yanga

WAKALA wa mchezaji wa Simba, Mnyarwanda, Meddie Kagere ambaye ni Patrick Gakumba, amefunguka na kusema mazungumzo kati yake na mabosi wa Yanga yanakwenda vizuri na kinachosubiriwa ni kukubali masharti aliyoipa timu hiyo kabla ya kusaini mkataba.

 

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu ziwepo tetesi za usajili wa mshambuliaji huyo kuwaniwa na Yanga katika usajili wa msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo imeandaa bajeti ya shilingi bilioni 1.5 za usajili.

Tuyisenge ni kati ya wachezaji wawili wanaotajwa kutua kusaini kuichezea Yanga akiwemo beki wa kati mahiri wa timu ya taifa ya Congo na Klabu ya AS Vita ya DR Congo, Yannick Bangala Litombo.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Gakumba alisema juzi aliwasiliana na viongozi wa Yanga kwa njia ya simu na kuwapa masharti mawili, kati ya hayo wamhakikishie mshahara wa kila mwezi kabla ya kusaini mkataba wa kuichezea timu hiyo.

Gakumba alitaja sharti lingine ni kukubali dau la fedha ambalo mchezaji wake atalitaka, hivyo kama masharti hayo watayatimiza, basi atatua kukipiga Jangwani katika msimu ujao.

 

Aliongeza kuwa, ametoa sharti hilo la mshahara kwa hofu ya mchezaji wake kutaabika baadaye baada ya kusaini Yanga na kikubwa hataki kuona mchezaji wake akipata matatizo hayo.

“Juzi niliongea na viongozi wa Yanga wakionyesha nia kubwa ya kutaka kumsajili Tuyisenge baada ya kuvutiwa naye, hivyo mazungumzo hayo yalikwenda vizuri lakini nimewapa masharti mawili ambayo wanatakiwa kuyatekeleza kabla ya kusaini mkataba.

 

“Moja, ni kumhakikishia mshahara wa kila mwezi baada ya kusaini mkataba huo na lingine wakubali kutoa dau ambalo mchezaji wangu atalitaka, hivyo kama hayo yote wakiyatekeleza, basi Tuyisenge anakuja Yanga.

“Nashukuru viongozi hao wamenihakikishia kuyatimiza hayo na kuniahidi kuwa hivi karibuni wanatarajiwa kupata mdhamini wa timu hiyo, hivyo nisiwe na hofu,” alisema Gakumba.

Hata hivyo, Gakumba aligoma kutaja dau la usajili wala mshahara wanaotaka kwa kuhofia kuharibu dili, akisisitiza ni mpaka watakapokutana uso kwa uso na viongozi wa Yanga.

Comments are closed.