The House of Favourite Newspapers

Tuzo za SZIFF Kufanyika Mlimani City Februari 23

Tuzo za Sinema Zetu (SZIFF) za kuwapata washindi zinatarajiwa kufikia kilele chake Februari 23 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam ikiwa sasa ni  takribani mwezi mmoja na nusu filamu hizo zilizochaguliwa zikionyeshwa katika chaneli ya Sinema Zetu kupitia Televisheni ya Azam.

 

Mratibu wa Tamasha hilo Bi, Sophia Mganza, amesema kuwa washiriki waliokidhi vigezo kwa mwaka huu wamekuwa na mafanikio makubwa baada ya filamu nyingi kutoka mikoa mbalimbali  tofauti na mwaka jana.Pia wamejipanga ili kuweza kufika katika mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani.

 

“Ubora wa kazi za filamu umekuwa mkubwa tofauti na ilivyokuwa mwaka jana katika tuzo za SZIFF 2018, na kwa upande wa filamu za kiswahili  filamu zilikuwa 141 na ambazo ziliingia  duru la pili ni 28 tu.

 

“Filamu fupi zilikuwa 73 na kati ya hizo ni filamu 11 ndizo ambazo zimeingia katika duru la pili, na tamthilia zilikuwa 20 na zilizoingia kwenye duru ni filamu 7 tu na makala zilizopita ni tatu na kuwa idadi ya filamu katika kila kipengele imetofautiana kulingana na ushindani uliokuwepo kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa katika upatikanaji wa washiriki.

 

“Tunaomba waendelee kupiga kura na pia wachague wasanii wanaostahili ambao filamu hiyo inaweza kuonekana Kimataifa,”alisema Mganza.

 

Naye Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Prof. Martini Mhando amesema upatikanaji wa washiriki katika kila kipengele ulizingatia vigezo vingi, na kwamba filamu zilizoshinda katika duru hilo la pili ni zile zenye ubora wa hali ya juu.

 

“Filamu ambazo zimeshinda vigezo vyote zimeangaliwa ikiwa ni pamoja muandishi bora, mpiga picha na kila ambacho kinatakiwa,”alisema.

 

Usiku wa tuzo hizo mgemi rasmi atatoa  tuzo kwa washindi na shilingi milioni moja hadi milioni tano zitatolewa ikiwa pamoja na vyeti.

 

Wasanii wakiume ambao wameingia katika kinyang’anyiro hicho ni Hemedi Suleiman, Salim Ahmed, Madebe Lidai, Maulidi Ally, Peter Paul, Mack Daim, Sango Johanes, Salumu Mpoyoka, Rashidi Msigala na Hasan Kazoa.

 

Wasanii wakike ni Jennifer Temu, Zaudia S Rajabu, Yvonne Cherries, Sifa Matanga, Asha Yassin Mussa, Wema Isaac Sepetu, Rhoida Richard, Flora Kihombo, Seba Sebastion na Blandina Chagula.

 

 

Stori: Neema Adrian na Memorise Richard.

Comments are closed.