The House of Favourite Newspapers

Twaha Kiduku: Mwakinyo Ananiogopa

0

BONDIA Twaha Kassim ‘Kiduku’ ambaye makazi yake yapo Kihonda, Morogoro ni moja kati ya mabondia wenye rekodi hapa nchini.

Rekodi ya mwisho aliipata baada ya kumchapa kwa TKO ya raundi ya saba Mthailand Sirimongkhon Lamthuan kwenye pambano la ubingwa wa WBC lililopigwa kwenye Ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar.

Ikumbukwe kuwa pambano hilo ni la pili kwa ukubwa Kiduku kushinda baada ya awali kumchapa Abdallah Pazi ‘Dullah Mbabe’ kwenye pambano la kumsaka Mfalme wa Wazaramo lililofanyika mkatika Uwanja wa Uhuru, Dar.

 

Championi Ijumaa limefanya makala na Kiduku kuhusiana na mambo mbalimbali kuhusiana na mchezo huo wa ngumi na anafunguka kama ifuatavyo;

Ni kweli ulinunua pambano lako na Mthailand kama inavyosema?

“Hapana, mimi ni bondia kwa nini ninunue pambano na hakuna kitu kama hicho. Promota alitafuta pambano akaniambia kwa hiyo mimi sijanunua pambano.

 

BAADA YA PAMBANO LILE KIPI KITAFUATA?

“Mwezi wa kumi na mbili nitakuwa na pambano na Mkongo ila sijamjua ni nani. Nina imani nitazidi kufanya vizuri na kuweza kuwapa furaha mashabiki zangu.

Ilikuwaje mpaka ukajijua unaweza kuwa bondia?

“Mimi nilikuwa napenda kupigana tangu nikiwa mtoto ndipo nikaamua kuifanya kama kazi yangu, ila kuna bondia hapa Morogoro anaitwa Nasibu au Baba Pili, ndiye aliyekuwa ananivutia sana kwa upiganaji wake na ndiye aliyeanza kunifundisha ngumi.

 

INASEMEKANA MKIENDA NJE KUPIGANA MNAUZA PAMBANO NI KWELI?

“Hapana kwa kweli mimi hili ndiyo nasikia kwako, na labda ni kweli ila mimi kwa upande wangu sijawahi maana naamini ile ndio nafasi nzuri ya kuonyesha uwezo wangu na hao wanaouza basi hawana matarajio makubwa na ngumi.

 

PAMBANO LAKO LA KWANZA ULILIPWA BEI GANI?

“Pambano langu la kwanza nililipwa elfu ishirini ilikuwa mwaka 2013, ilikuwa ndogo ila walau ilinifariji kuweza kuzidi kujitahidi.

 

PAMBANO GANI ULILIPWA FEDHA NYINGI?

“Ilikuwa nilipoenda nchini Poland, nilipewa milioni 22, nilifurahi sana kwani niliona faida ya ngumi.

Ulishawahi kuwaza kuzichapa na Mwakinyo?

“Ndiyo na niliomba pambano naye ila sikupata mrejesho wowote, labda ananiogopa na pia siwezi kulazimisha kama mtu hataki ila mimi nilitaka kujipima tu na yeye.

 

KWENYE SOKA UNASHABIKIA TIMU GANI?

“Mimi ni shabiki mkubwa wa Simba na naipenda.

Mchezaji gani wa Simba unampenda?

“Navutiwa na uchezaji wa wachezaji wengi wa Simba ila nahodha John Bocco navutiwa naye sana kuliko wote.

 

HIVI UMEOA?

“Hapana bado sijaoa ila Mungu akijalia nitaoa.

Ikija ikatokea mwanao akatamani kuwa bondia, utamruhusu?

“Inategemea kama ngumi itakuwa kipaji chake basi nitamruhusu na kumpa sapoti kubwa ila kama atakuwa na kipaji kingine nitampa sapoti pia kwani sio lazima na yeye awe bondia kama mimi.

 

KITU GANI CHA AJABU KIMEWAHI KUKUTOKEA UKIWA ULINGONI?

“Kwa upande wangu hakipo na kama kipo basi mimi nakiona cha kawaida tu.

 

NGUMI ZIMEKUPA MANUFAA GANI MPAKA SASA?

“Ngumi zimenisaidia mambo mengi sana ya kiuchumi kwani imeniwezesha kufungua biashara ndogondogo za kujikimu kimaisha na hata hapa nilipo ni kwa uwezo wa ngumi.

 

USHAWAHI KUTAMANI KUCHEZA NJE YA NCHI?

“Ndiyo nishawahi kutamani kwani ni ndoto ya kila bondia. Ilikuja dili kutoka Marekani nisaini miaka mitano ili nikacheze huko, nikakataa kwani niliona haitakuwa na manufaa sana kwangu kwani waliniambia kwa mwaka nacheza mapambano mawili na kila pambano dola 250, kama milioni 5 tu.

“Nikashauriana na uongozi wangu nikaona ni bora nibaki nyumbani,” anamaliza Kiduku.

CAREEN OSCAR,

Dar es Salaam

Leave A Reply