The House of Favourite Newspapers

Twaweza: Asilimia 79 ya Wananchi Hupata Huduma za Fedha Kupitia Simu

twawezaUTAFITI wa Taasisi ya Twaweza umeonyesha kuwa asilimia 79 ya wananchi wanatumia huduma za fedha kupitia mitandao ya simu za mkononi na wanaridhishwa na huduma zinazotolewa.

Wakati huohuo wananchi walipoulizwa kuhusu suala la gharama za huduma za fedha kwenye mitandao ya simu za mkononi, watu wanne kati ya kumi (asilimia 38) walisema gharama hizo ni kubwa mno.

Hayo ameyasema leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze, alipokuwa akizungumza na wanahabari na kusema utafiti huo unatokana na muhtasari wake uitwao “Fedha, fedha, fedha! Wananchi na huduma rasmi za kifedha”.

Alieleza kwamba mbali na kuwa muhtasari, unatokana na takwimu za sauti za wananchi za utafiti wa kwanza barani Afrika kwenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mkononi.

Alifafanua kuwa idadi ya watu wazima wanaotumia huduma za kifedha kupitia simu za mkononi imeongezeka kutoka asilimia 61 mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 80 mwaka 2016.

“Hii inamaanisha kwamba lengo la serikali la kufikisha huduma za kifedha kwa asilimia 50 ya Watanzania ifikapo mwaka 2016,  limepitwa kwa kiasi kikubwa.

“Utafiti huu wa sauti za wananchi umeonyesha kwamba kuongezeka kwa idadi ya waliofikiwa na huduma hizi ni dalili njema na ifahamike kuwa wahojiwa wa sauti za wananchi hupewa simu za mkononi ili kufanikisha zoezi la kupata takwimu sahihi zisizo na ubaguzi,” alisema Eyakuze.

Aliongeza kuwa takwimu hizo zilikusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,800 wa maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara tu pasipo kuhusisha Zanzibar, kuanzia Septemba 14 hadi 26, mwaka huu.

Na Denis Mtima/GPL

Comments are closed.