Twendeni kwa wingi Taifa tukaisapoti Stars leo
TAIFA Stars inakipiga jioni ya leo kwenye Uwanja wa Taifa. Inacheza na Burundi katika mechi ya kuwania kufuzu Kombe Dunia. Ni mechi ngumu na muhimu kwa Stars ambayo katika mechi ya awali walitoka sare ya bao 1-1, hiyo ikimaanisha kwamba tunahitaji japo suluhu kwenye Uwanja wetu ili tufuzu katika makundi ya kuwania kwenda Kombe la Dunia Quatar.
Ni mechi muhimu ambayo kwa aina ya wachezaji tulionao na mahitaji ya soka letu kwa sasa tuna kila sababu ya kushinda na kukuza ubora wetu kwenye soka la Afrika. Kaimu Kocha Mkuu wa Stars, Ettiene Ndayiragije amepanga kikosi imara na leo ni vita tu ndani ya Uwanja wa Taifa mpaka kieleweke. Hatupaswi kutafuta suluhu twende tukawashangilie Stars washinde tuwe na uhakika.
Kila Mtanzania anapaswa kujipanga vilivyo kutoa sapoti ya hali na mali ndani na nje ya Uwanja kufanikisha mechi hiyo muhimu ya leo.
Mashabiki na wadau wengi wameonekana kufurahishwa na uteuzi wa kikosi cha Stars hivyo ni wakati muafaka kwenda Taifa kuishangilia timu yetu ili tutimize lengo letu na kuwarahisishia kazi wachezaji wetu. Huu ndiyo wakati wetu.
Huu siyo muda wa kulumbana ni muda wa kuungana na kusapoti wachezaji wetu kuhakikisha kwamba timu yetu inafuzu kucheza michuano hiyo ya Kombe la Dunia ambayo ina heshima kubwa zaidi Duniani kwenye soka la ngazi ya timu ya Taifa. Tupambane hatua kwa hatua na vijana wetu mpaka dakika ya mwisho kama ilivyokuwa wakati tunawania kufuzu Afcon. Tukianza migawanyiko na kunyoosheana vidole kwa misingi ya ushabiki wa timu hii na ile au mchezaji huyu na yule hatuwezi kujenga wala kufanya kitu cha maana.
Tuvae jezi zetu kwa wingi tumiminike ndani ya Uwanja wa Taifa kukamilisha dhamira yetu na tunaamini wachezaji wetu kwa mzuka waliotuonyesha hawatatuangusha.
Tunaamini kikosi ambacho ametaja kocha kitakuwa msaada kwa taifa na kitafanya vizuri kwenye mchezo wa leo na kujiwekea mazingira mazuri ya hatua inayofuata kwani hatma yetu iko mikononi mwetu. Kila mmoja anapaswa kuelewa kwamba tunahitaji ushindi kwa namna yoyote ile ili kufuzu na kwa aina ya timu Burundi waliyonayo tunahitaji mshikamano mkubwa sana ndani na nje ya uwanja.
Burundi ina wachezaji wenye uzoefu na waliokuzwa kwenye misingi mizuri ambao wanaijua vilivyo Tanzania na ushindani uliopo nje ya uwanja baina ya timu hizo mbili, hivyo tusipokuwa na mshikamano tunaweza kujikwamisha wenyewe kwavile mechi na matokeo bado yako wazi.
Kila kitu kipo mikononi mwetu. Itakuwa ni aibu sana kama tutashindwa kuujaza uwanja wa Taifa haswa ukizingatia kwamba leo hakuna mchezo wowote mkubwa na wa muhimu nchini zaidi ya kupambania mashujaa wetu.
Twendeni Taifa tukapambane kwa pamoja kutetea heshima ya Tanzania, sare ambayo vijana wetu walipambana na kuipata kwenye mazingira magumu ya ugenini tukawaonyeshe kwamba tunaithamini na tunatambua juhudi na mapambano yao.
Comments are closed.