The House of Favourite Newspapers

Ubahili huu hadi kwa wazazi na ndugu zako utakusaidia nini?

0

young-couple-arguing-on-a-sofa-136381366849303901-130702114836Mwishoni mwa wiki iliyopita nilikuwa kijijini kwetu Mlalo, Lushoto mkoani Tanga ambako nilikuwa na matatizo kidogo. Niliposhuka tu stendi, nilikutana na baadhi ya marafiki zangu wa muda mrefu ambao waliponiona walionesha kufurahi kupitiliza.

Nilidhani walikuwa na furaha baada ya kuniona kwani tuliachana muda mrefu uliopita, lakini haikuwa hivyo! Walijua kufika kwangu pale, neema imewashukia. Basi unaambiwa kila mmoja alikuwa akitaka nimpe pesa.

Kwa kifupi mimi siyo mbahili, ni mtu wa kutoa pale ambapo nastahili kutoa. Kwa kuwa nilikuwa na vijisenti mfukoni, nilitoa shilingi 10,000, nikawataka vijana hao watatu wagawane. Walinishukuru sana na mmoja wao aliniambia kwa kuninong’oneza kuwa nimemuokoa kwani alikuwa na hali mbaya.

Lakini nikiwa pale kijijini nikapata malalamiko kuwa, kuna baadhi ya watu wakienda huko wanakuwa wabahili. Si watu wa kutoa licha ya kwamba wanaonekana mambo yao ni supa.

Kufuatia malalamiko hayo, nikaona leo nizungumzie jambo moja! Ubahili walionao baadhi ya watu hadi kwa wazazi na ndugu zao. Sikatai, ili uwe na mafanikio kwenye maisha ya sasa, unatakiwa kuwa makini sana na kila shilingi unayoipata.

Ile tabia ya kutoatoa pesa kwa kila mtu anayekuomba inaweza kukufanya ukaishia kupata sifa nyingi kwamba ni mtu wa kutoa sana lakini usiwe unafanya mambo ya msingi.

Kuna watu ambao wakiwa baa, kila anayeomba ofa anapewa. Wengine wanasifika kwa kuhonga wakidai pesa ni makaratasi tu!

Niseme kwamba, kutoatoa pesa kiholela kutakupa sifa za kijinga lakini hakuwezi kukusaidia katika maisha yako. Hivyo basi, unapotoa pesa na kumpa mtu, iwepo sababu ya msingi ya kufanya hivyo.

Lakini ninapozungumzia ishu ya kuwa na nidhamu na pesa, simaanishi kwamba uwe bahili kabisa. Wapo watu ambao kwa sababu wana malengo makubwa kwenye maisha yao, wanakuwa bahili hata kwa ndugu zao wa karibu.

Mtu anakuwa bahili hadi kwa wazazi wake, anashindwa kuwasaidia pale wanapomlilia shida, kisa eti pesa zake anataka kujengea nyumba au kununulia gari. Hii siyo sawa hata kidogo!

 Pale unapojaaliwa kuwa na kipato kizuri, una jukumu la kuwasaidia ndugu zako wakiwemo wazazi wako pale wanapokulilia shida. Wasaidie pale inapobidi kwa kuwa, kususa kuwasaidia wakati wanakutegemea ni kujiweka katika mazingira ya kukosa baraka zao.

 Nasema haya kwa sababu, wapo watu ambao kutokana na ubahili wao, achilia mbali ndugu zao na wazazi wao, wanakuwa wabahili hata kwa familia zao.

Watoto na wake zao wanaishi maisha ya ajabu, kula kwa shida na hata nyumba wanayoishi haina hadhi yao lakini mwanaume ana pesa, ziko benki zinasubiri kufanyia mambo makubwa. Sasa unajiuliza, kuna mambo gani makubwa ya kuzifanyia pesa zako zaidi ya kuifanya familia yako iishi vizuri?

Huo ni ulimbukeni! Kama Mungu kakujaalia uwezo, jua kwamba yeye kafanya hivyo ili uweze kuwasaidia wengine wasio na uwezo. Ndiyo maana tunaambiwa tuwasaidie yatima, tutoe sadaka na zaka, kwa nini? Kwa sababu kutoa kwako huko ndiko kutawasaidia wengine wanaotegemea kuishi kupitia kipato chako.

Nihitimishe kwa kusema tu kwamba, ubahili siyo kitu kizuri ila unatakiwa kuwa na nidhamu ya pesa zako. Wasaidie wenye uhitaji! Ndugu zako na familia yako wasiishi maisha magumu wakati pesa unayo.

Ila wale wanaokupiga mizinga ili wakafanyie anasa, usiwe mgumu kuwakatalia hata kama ni ndugu, jamaa au marafiki zako.

Leave A Reply