UBAKAJI WATIKISA DAR WANAWAKE WACHARUKIA POLISI, WASEMA: TUMECHOKA!

TUMECHOKA! Ndivyo walivyosikika kundi kubwa la wanawake ambao wameandamana kupinga tukio lililowatikisa la ubakaji wa binti wa miaka 16 anayedaiwa kubakwa na mjomba wake, UWAZI lilikuwepo.  Wanawake hao walifunga Mtaa wa Bwawani Maramba- Mawili, Mbezi jijini Dar, mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kushindwa kuvumilia tukio la mtoto huyo kudaiwa kubakwa na mume wa shangazi yake (mjomba wake) aliyetajwa kwa jina moja la Kipengele.

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, Kipengele alidaiwa kumfanyia binti huyo ukatili huo wa kingono na kumharibu vibaya sehemu zake nyeti kiasi cha kushindwa kutembea kutokana na maumivu makali.

SIMULIZI YA KUSIKITISHA

Akilisimulia Gazeti la Uwazi mkasa huo wa kusikitisha huku akiwa na maumivu makali sehemu za siri, binti huyo ( jina linahifadhiwa kwa sababu za kimaadili) alisema siku ya tukio hilo alikwenda kumsalimia shangazi yake ndipo akakutana na dhahama hiyo. Alisema alipofika nyumbani kwa shangazi yake, Kipengele alimuita na kumuingiza chumbani kisha kumfanyia ukatili huo.

“Nilikwenda kumsalimia shangazi yangu kwa sababu ninaishi na baba na mama wa kambo (wote wanaishi Bwawani, Maramba-Mawili).

“Nilipofika nilimkuta mume wa shangazi ambaye huwa ninamuita babu kwa sababu umri wake ni mkubwa (anakadiriwa kuwa na umri wa miaka 60 na kuendelea). “Nilipomuuliza shangazi yupo wapi, babu aliniambia alikuwa amekwenda Kinyenze (hukohuko Maramba-Mawili).

“Baada ya hapo mjomba aliniita, nikajua anataka kunituma, lakini nilishangaa kumuona ananishika mkono na kuniingiza chumbani kwake kwa nguvu. “Baada ya kuniingiza chumbani alianza kunivua nguo kinguvu kisha alinilaza kitandani. “Wakati bado ninashangaa nini kinatokea, mjomba alichukua mtandio wa shangazi na kunisokomeza mdomoni ili nisipige kelele.

“Baada ya kunishinda nguvu na kunikaba kwa kunijaza nguo mdomoni, alinibaka mara ya kwanza, akarudia mara ya pili na ya tatu bila kujali maumivu niliyokuwa ninapata. “Baada ya hapo alinivalisha nguo ya ndani na kunitoa nguo mdomoni kisha aliniachia akaniambia nisimwambie mtu yeyote kitendo alichonifanyia.

MAUMIVU YAZIDI

“Niliporudi nyumbani sikumwambia mtu kutokana na woga lakini nilipoona maumivu yananizidi, nilimwambia mama, lakini hakuchukua hatua yoyote hivyo ilibidi nimwambie mwalimu wangu. “Baada ya kunisikiliza, mwalimu alikwenda kuwaeleza viongozi wa Serikali ya Mtaa. “Kweli viongozi wa Serikali ya mtaa walimuita mjomba, lakini hakwenda,” alisema binti huyo huku akiangua kilio.

BABA MKUBWA AZUNGUMZA

Akizungumzia tukio hilo, baba mkubwa wa binti huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la Omary alisema alipigiwa simu na majirani akiwa safarini Dodoma ambapo walimweleza kuwa mtoto wa mdogo wake alikuwa amebakwa na Kipengele.

“Nilichokifanya nilimpigia simu mdogo wangu na kumuuliza kuhusu taarifa za binti yake kubakwa, lakini aliniambia anaumwa na alikuwa anasubiri barua kutoka Serikali ya mtaa kuhusu tukio hilo. “Baada ya pale niliagana na mdogo wangu kwa makubaliano kuwa atanijuza kitakachojiri.

“Nilipoona mdogo wangu yupo kimya ilibidi nirudi Dar, nikakutana na mdogo wangu kisha nilimuuliza analichukuliaje suala hilo? “Niliona kama mdogo wangu ananizungusha kiasi cha kupandwa na hasira. “Niliamua kumfuata dada yangu ambaye mumewe ndiye anatuhumiwa, nikagombana naye kwa sababu niliona alishindwa hata kumpeleka mtoto hospitalini.

“Kumbe wakati huo yule binti alikuwa amewapa taarifa hizi marafiki zake ambao nao waliwaeleza mama zao ambao waliamua kuandamana kupinga tukio hilo la unyanyasi wa kingono kwa mtoto. “Wale wanawake walikuwa wanashinikiza Serikali ya mtaa impeleke Kipengele polisi,” alisema baba mkubwa huyo.

MAJIRANI

Mmoja wa majirani aliyezungumza na UWAZI juu ya tukio, Suzana Steven alisema alipata taarifa ya kutokea kwa tukio hilo kutoka kwa marafiki wa binti huyo. “Ilibidi niongee na wanawake wenzangu juu ya suala hili na kiukweli kila mmoja alionesha kuchukizwa na tukio hili.

“Tuliamua kuandamana ili kulishinikiza jeshi la polisi Dar chini ya Kamanda Lazaro Mambosasa (Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar) kuchukua hatua stahili kwa mtuhumiwa ili kukomesha vitendo hivyo,” alisema mama huyo.

KIPENGELE ASAKWA

Kwa upande wake viongozi wa Serikali ya mtaa walithibitisha kupokea malalamiko na kuwepo kwa maandamano ya wanawake hao huku mtuhumiwa akiendelea kusakwa baada ya taarifa zake kuripotiwa polisi.

“Taarifa hizi zipo polisi na mtuhumiwa anatafutwa ili aweze kuhojiwa na polisi, yeyote atakayemuona popote, atujulishe ili akamatwe,” alisema kiongozi mmoja wa serikali ya mtaa ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa siyo msemaji.

Waandishi: Neema Adrian na Athmani Hamisi (SJMC).


Loading...

Toa comment