The House of Favourite Newspapers

Ubinafsi; Kirusi hatari kwa wapendanao!

0

shutterstock-couple-huggingTUMSHUKURU Mungu wa Mbinguni kwa kuendelea kutupa pumzi ambayo hatuilipii hata senti moja. Mimi na wewe tunakutana kwa mara nyingine tena katika ukurasa wetu huu maridhawa wa love story, tunajifunza kwa pamoja.

Kwa wale tuliokuwa pamoja wiki iliyopita, tulijifunza vitu mbalimbali vya kumfanyia mpenzi wako kabla ya kusema; mwanaume hata umpe nini haridhiki. Niwashukuru wale wote waliosoma na kunitumia ujumbe kwamba wamependa mada na kujifunza kitu.

Leo tutaitazama mada iliyopo kwenye kichwa cha habari. Ubinafsi ni kirusi hatari katika uhusiano. Kuna msemo wa Kingereza unaosema; ‘The one who not can give also will never receive.’ Msemo huo una maana pana sana katika suala zima la uhusiano.

Uhusiano wowote wa mapenzi unakuwa imara kutokana na ushirikiano. Ushirikiano unapaswa kuwa wa pande mbili. Mwanaume anapaswa kushirikiana na mwanamke, vivyo hivyo mwanamke, anapaswa kushirikiana na mwanaume.

Hiyo ndiyo maana halisi ya pendo. Ndipo msemo huo unapokuwa na maana kamili. Ili mwenzako aendelee kukupa, huna budi na wewe kumpa. Mtu unapaswa kumpenda mwenzako ili naye akupende. Usitegemee ukawa unajipenda mwenyewe tu halafu mwenzako awe anakupenda wewe.

Penzi linanoga pale kila mtu anapoonesha ushirikiano kwa mwenzake. Pendo linakamilika pale kila mmoja anapomthamini mwenzake. Mjali mpenzi wako kadiri ya nguvu, uwezo na maarifa yako yote ili naye afanye vivyo hivyo kwako.

Kama mpenzi wako anawajali ndugu zako, kwa nini wewe usiwajali wa kwake? Anapowajali ndugu zako, anapowatendea mazuri ndugu zako, hakika anakufurahisha wewe hivyo na wewe huna budi kuwatendea mazuri ndugu zake.

Unapomuona mpenzi au mumeo anawajali ndugu zako kwa kuwaulizia wanaendeleaje, kutaka kujua kama ni wazima au wanaumwa, kutaka kuwasaidia pale wanapokuwa na tatizo, usisubiri  kuambiwa. Tambua kwamba na wewe una wajibu wa kuwajali ndugu wa mumeo.

Ndiyo maana mafundisho mengi ya masuala ya ndoa yanaelekeza, mwanamke anapoolewa, anapaswa kuwajali zaidi wakwe au ndugu wa mume wake. Mume anashauriwa zaidi kuwajali ndugu wa mkewe. Yote hiyo inafundishwa ili kukamilisha neno upendo.

Yanasaidia kuondoa ile dhana ya kujipenda mwenyewe. Yanaelekeza hivyo ili kuleta usawa. Ni kawaida mtu kuwapenda ndugu zake lakini wakati mwingine huwa ni vigumu kidogo kuwapenda ndugu wa upande wa pili.

Mnapoungana katika ndoa, mbali na kuungana nyinyi wanandoa, mnaunganisha koo zote mbili. Hivyo mbinu rahisi ya kuunganisha koo hizo, ni mwanaume kuwajali, kuwathamini ndugu wa mwanamke ambao anakuwa hajawazoea.

Mwanamke anapaswa kuweka jitihada kuwapenda ndugu wa mume ambao pia anakuwa hajawazoea. Akifanikiwa hilo na mwanaume naye akafanikiwa, watakuwa wameshaunganisha koo mbili ambazo zitashirikiana, zitashibana kwa hali na mali.

Unapoona mwenzako anakupa zawadi nzuri na wewe ukaifurahia, tambua kwamba utakapompa zawadi na yeye hata kama ni ndogo, ataifurahia. Si lazima kwamba umpe zawadi katika kiwango kilekile alichokupa lakini hata kama ni kidogo, unapompa mwenzako naye ataona unamthamini.

Usiwe mtu wa kupokea tu kila siku. Unapaswa na wewe kutoa. Mwenzako amekuletea zawadi ya viatu vizuri, siku nyingine wewe waweza kumnunulia hata soksi lakini akafurahi sana. Ataona unamjali. Usimtegee mwenzako. Umpe kadiri uwezavyo bila kujali yeye amekupa nini.

Ukiona mwenzako anakujali unapoumwa au kupata matatizo yoyote, huna budi na wewe kumjali pale na yeye anapopata matatizo. Usiwe mtu wa kuishi na mwenzako pale anapokuwa mzima au anapokuwa na raha, akiwa na huzuni wewe unakaa pembeni. Shirikianeni katika shida na raha, uzima na hata magonjwa.

Kwa leo tuishie hapo, tukutane tena wiki ijayo Mungu akipenda kwa mada nyingine nzuri. Usikose!

KUNUNUA NA KUSOMA MAGAZETI YA GLOBAL PUBLISHERS ONLINE, INGIA HAPA==>VODACOM M-PAPER APP

*********

JIUNGE NA SOCIAL MEDIA ZETU

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA

INSTAGRAM: @Globalpublishers

ERIC SHIGONGO INSTAGRAM: @ericshigongo

TWITTER: @GlobalHabari

FACEBOOK: @GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE: Global TV Online

GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, ERIC SHIGONGO FACEBOOK PAGE:@shigongotz

Leave A Reply