The House of Favourite Newspapers

Ubunge wa Harmonize Tandahimba Njia Panda

0

Oktoba 15, 2019, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli ‘JPM’ alitamka kuwa anatamani staa wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’, agombee ubunge kwenye jimbo analotokea la Tandahimba.

 

Magufuli alitoa kauli hiyo kwenye mkutano wa hadhara mjini Ruangwa mkoani Lindi ambapo Harmonize au Harmo alitumbuiza.Ishu hiyo iliibuka tena Jumanne wiki hii wakati Rais Maguli akifunga Bunge la 11, tayari kwa viongozi wote kurejea kwenye majimbo yao.

 

“Jamani vipi sasa kuhusu huyu ndugu yetu Harmonize? Maana mwaka jana mzee baba alimuelewa, sasa tunategemea mwaka huu aende na yeye huko jimboni kwao akachukue fomu ili awaongoze wananchi wake,” alichangia mdau mmoja mtandaoni.

 

Hata hivyo, kila mtu alionekana kuongea lake huku wengine wakisema staa huyo hawezi kuongoza, hivyo abaki tu kwenye muziki ndicho kitu anachokiweza na siyo kwenda kuwa kiongozi, kwani hatafanya vizuri na mwisho wa siku atapoteza mashabiki wake wa muziki.“Jamaa abaki tu hukuhuku (kwenye muziki) ndipo kunamfaa.

 

Huko kwenye uongozi hataweza, halafu mwisho wa siku atajikuta anapoteza mashabiki alionao,” alichangia shabiki mwingine aliyefahamika kwa jina la Juma.

 

Ili kujua kinachoendelea kwa upande wa Harmo, Gazeti la IJUMAA lilimvutia waya meneja wake, Beauty Mmary ili kujua wao kama viongozi wamejipanga vipi na kama kuna taratibu tayari zimeanza kufanyika, basi aseme na haya ndiyo yalikuwa majibu yake;“Harmonize hajachukua fomu yoyote, lakini pia mimi naona tubaki kwenye ileile kauli yake aliyoizungumza mwanzo, tusiweke tena maelezo mengine, kwa sababu alishazungumza msimamo wake kuhusu suala hilo, hivyo sifikirii kama ni sahihi kuendelea kulizungumzia.

 

“Alishatoa msimamo wake tangu mwanzo, kwa hiyo hata kama Bunge limevunjwa na watu wamerudi majimboni, lakini watu wachukulie msimamo uleule ambao aliusema tangu mwanzo.

 

“Kuna taarifa zinasambaa kuwa, Harmonize kakubali kugombea ubunge, siyo za kweli kwa sababu siku ambayo anafanya interview nilikuwa naye na ilikuwa ni shoo ya live, hivyo kwenye kumbukumbu zangu sikumbuki sehemu ambayo alisema atagombea au hatagombea.

 

“Lakini alizungumzia jinsi alivyochukulia suala la Rais kumpointi na kumuweka kwenye hiyo nafasi na anaionaje thamani yake kwenye muziki na kazi anayofanya kama kijana, lakini siyo mambo mengine.“Sisi kama menejimenti, kuna vitu ambavyo ni vya ndani sana, hatuwezi kuviweka hadharani. Hivyo, hatuwezi kusema kwa sasa msimamo wetu ni upi kuhusu msanii wetu kwenda kugombea Ubunge jimboni kwao, ila likitokea tutalizungumzia kama menejimenti,” alisema Beauty.

Stori: MEMORISE RICHARD, Ijumaa

Leave A Reply