The House of Favourite Newspapers

Ubunifu wa FinTech na Biashara Changa Kupitia “Wazo Challenge” Wahamasishwa

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser ( wa pili kulia) akizungumza na Muanzilishi Mwenza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Hindsight Ventures, Bw. Ajay Ramasubramaniam (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Huduma za kibenki Kidigitali kutoka Absa Group, Bw. Tawanda Chatikobo (kushoto), na Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja na Huduma za Kidigitali, Bw. Samuel Mkuyu, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa Wazo Challenge unaolenga kuimarisha ubunifu na ujasiriamali katika sekta ya Teknolojia ya Fedha (FinTech) na biashara changa (startup) nchini Tanzania.
Dar es Salaam 23 Machi 2025: Benki ya Absa Tanzania, kwa kushirikiana na Hindsight Ventures, imezindua Wazo Challenge Tanzania, mpango wa kipekee unaolenga kuimarisha ubunifu na ujasiriamali katika sekta ya Teknolojia ya Fedha (FinTech), na biashara changa (startup) nchini Tanzania.
Hafla ya uzinduzi, iliyofanyika  jijini Dar es Salaam jana na kuhudhuriwa na Mgeni Rasmi, Bw. Kennedy Komba, Mkurugenzi wa Huduma Jumuishi za Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania, akimwakilisha Gavana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango wa Wazo Challenge Tanzania.
Ikiwa na kaulimbiu “Benki ya Siku Zijazo” au “Bank of the Future”, Wazo Challenge Tanzania inakaribisha biashara changa katika Teknolojia ya Fedha za (FinTech) na wabunifu kuwasilisha suluhisho bunifu zinazoweza kufanikisha mabadiliko makubwa katika sekta ya kibenki.
Mpango huu ni sehemu ya ushirikiano wa miaka mitatu kati ya Benki ya Absa Tanzania na Hindsight Ventures, ukiwa na lengo la kusaidia ukuaji wa ujasiriamali na kuongeza upanuzi wa startups nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Bw. Obedi Laiser, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, alisisitiza dhamira ya benki hiyo katika kukuza ubunifu na ujumuishaji wa kifedha.
“Wazo Challenge Tanzania ni uthibitisho wa imani yetu katika nguvu ya ubunifu kwenye kuleta maendeleo na thamani kwa wateja wetu – na hii inaenda sambamba na lengo kuu la benki yetu ikiwa ni “Kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja, hatua moja baada ya nyingine.” na Ahadi ya chapa yetu “Stori yako ina thamani”. Tunafurahia kushirikiana na Hindsight Ventures kuwawezesha wabunifu na wajasiriamali wa Tanzania.”
Bw. Ajay Ramasubramaniam, Mwanzilishi Mwenza na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hindsight Ventures, aliunga mkono kauli hiyo, akisema, “Tunatarajia kufanya kazi na Benki ya Absa Tanzania ili kuimarisha mfumo wa FinTech wa ndani kupitia mbinu iliyopangiliwa ya kugundua na kushirikiana na bidhaa na suluhisho bunifu.
Startups na wabunifu watanufaika kwa kupata ufikiaji wa mtandao wa Absa, pamoja na mtandao wetu wa kimataifa wa FinTech, na tunahisi kuwa hii itakuwa hatua muhimu kwa sekta hii.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma Jumuishi za Fedha  kutoka Benki Kuu ya Tanzania, Bwana Kennedy Komba, akimwakilisha Gavana, alipongeza benki ya Absa Tanzania kwa kuja na Wazo Challlenge huku akisema ni moja ya njia ya kuhamashisha matumizi ya teknolojia nchini.
“Tumetazama masuala ya teknolojia na tumeona bila teknolojia, sekta ya fedha haiwezi kuendelea vizuri, Kuna mambo tunaona huduma za kibenki zinaweza kubadilika katika miaka mingine 10 ijayo, sambamba za serikali katika kuangalia tunakuea na uchumi wa kidigitaliz moja wapo ni data ama taarifa za mtumiaji kwamba zinatakiwa zilindwe na kutumika kwa ajili ya kukuza huduma mbalimbali.
“Tumeangalia fursa zilizo mbele kuweka mazingira wezeshi ya kuweza kuwasaidia wanateknolojia ama wabunifu waweze kupata hizi huduma za fedha kulingana na kanuni za udhibiti zilizowekwa na Benki Kuu, Ili waweze kuingiza bidhaa zao sokoni kupitia mazingira rahisi na wezeshi”, alisema Bw. Komba.
Aidha alisema BoT ina imani Benki ya Absa kupitia Wazo Challenge Tanzania itaongeza fursa kwa vijana na kutoa huduma bora zinazoendana na uhitaji wa soko la Tanzania huku changamoto zilizopo zikitatuliwa na watanzania wenyewe.
Mpango huu unalenga kufanya huduma za benki kuwa rahisi zaidi na zinazozingatia mahitaji ya wateja, kwa kutumia maendeleo ya mabadiliko ya kidijitali ili kukidhi matarajio ya wateja wa kisasa.
 Mpango huu pia utatoa fursa kwa biashara changa za teknolojia ya fesha kushirikiana na Benki ya Absa Tanzania kupitia ushauri, ushirikiano, na uwekezaji. Kuingia kwenye mpango huu usio na ada kutategemea kukamilisha mchakato wa kufuzu na ukaguzi wa historia.
Zaidi ya hayo, Wazo Challenge Tanzania itatoa ufikiaji kwa wataalam wa sekta, wakufunzi, na washauri kusaidia wenye biashara changa katika safari yao ya kuanzisha na kukuza biashara zao. Mpango huu pia unalenga kuunganisha biashara changa zilizochaguliwa na mtandao wa kimataifa wa wataalam wa FinTech na wawekezaji, wanaotaka kusaidia ukuaji wa sekta ya Teknolojia ya Fedha nchini Tanzania.
Mfumo wa FinTech wa Tanzania umeendelea kukua kwa kasi, huku biashara kadhaa za ndani zikivutia uwekezaji wa mitaji na kushughulikia mahitaji ya wateja.
Programu kama Wazo Challenge Tanzania zina nafasi muhimu katika kusaidia mfumo huu, kwa kuhamasisha ubunifu katika suluhisho za fedha za kidijitali, ufadhili wa mnyororo wa ugavi, huduma za malipo, upimaji wa mikopo, na uwezeshaji wa mnyororo wa thamani.
Toleo la “Benki ya Siku Zijazo” la Wazo Challenge litahitimishwa kwa Siku Maalum ya Uoneshaji wa Ubunifu wa Kazi, itakayofanyika kwa mwaliko maalum, ambapo washindi wa fainali  watapata nafasi ya kuwasilisha suluhisho zao za FinTech mbele ya jopo la wawekezaji na viongozi wa sekta.
Wazo Challenge Tanzania itaendelea kutoka 2025 hadi 2027, huku Benki ya Absa Tanzania na Hindsight Ventures wakitoa programu za mafunzo, ushauri na ufadhili ili kuhakikisha mafanikio ya wenye biashara changa na wabunifu wanaoshiriki.