The House of Favourite Newspapers

Uchaguzi 2015…Magufuli, Lowassa mwisho wa ubishi!

0

magufuli (4)Mwandishi Wetu

Hatimaye zile mbio za Kampeni za Uchaguzi Mkuu 2015 zilizoanza Agosti 23, mwaka huu, leo zinafikia tamati ambapo wagombea wawili wenye msisimko wa aina yake, Dk. John Pombe Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Ngoyai Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wanafunga kazi katika Majiji ya Mwanza na Dar.

MAGUFULI MWANZA

Baada ya kumaliza kuzunguka mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani kisha kurejea jijini Dar akiunganisha na Mkoa wa Pwani, leo atalitikisa Jiji la Mwanza katika Viwanja vya Kirumba akifunga kampeni zake hizo.

Hadi anafunga kampeni zake hizo, Magufuli amefanya karibia mikutano 300 katika majiji, miji na vijiji mbalimbali nchini huku akijinadi kwa ilani ya chama chake aliyoahidi kuitekeleza kwa dhati kwa kubadili mfumo wa kiutawala.

Huku akitumia msemo wake wa ‘Hapa Kazi Tu’ na staili ya kupiga push up (Magufulika), kote alikopita alieleza baadhi ya vipaumbele vya serikali yake kuwa ni pamoja na kujenga umoja wa kitaifa, kulinda muungano, ulinzi na usalama, kuheshimu mihimili ya dola, kuanzisha mahakama maalum ya mafisadi na majizi, utawala bora, kuheshimu mawazo yote ya kuleta maendeleo hata yakitoka upinzani na kuimarisha vyombo vya usalama.

Vingine alivyoahidi ni vita dhidi ya ubadhirifu, kodi ilipwe na wote, kuongeza ajira kwa kuimarisha viwanda vya ndani, kufufua sekta ya kilimo, mifugo na tija kwa kujenga viwanda, kudhibiti madini, kupeleka maji vijijini na mijini, kujenga zahanati kila kijiji, hospitali ya rufaa katika kila mkoa na kuboresha maslahi ya wauguzi.

Vingine ni elimu ya bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne, kujenga nyumba za walimu, mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu, kujenga hosteli za wanavyuo, kuboresha maslahi ya watumishi na kusimamia gesi, kuboresha barabara, flyovers na reli.

Pia ameahidi kulinda haki za walemavu, uhuru wa habari, kulinda haki za wasanii na wanamichezo na nyingine nyingi hasa kulinda rasilimali za Tanzania.

Mheshimiwa huyo anatarajia kufunga kampeni zake kwa kishindo akiweka msisitizo katika vipaumbele hivyo huku akiambatana na timu kamili jijini Mwanza wakiwemo wasanii na viongozi mbalimbali wa CCM.

lowassaaLOWASSA JANGWANI

Kwa upande wake, mgombea wa Chadema, Lowassa anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ataisimamisha Dar katika Viwanja vya Jangwani kuhitimisha kampeni zake alizofungulia kwenye viwanja hivyo. Lowassa na timu yake amezunguka mikoa yote Tanzania Bara na visiwani huku akikutana na mafuriko ya Wana-Ukawa waliokuwa wakijinasibu kuwa wanataka mabadiliko.

Katika ziara zake, Lowassa alivitaja vipaumbele vya serikali yake kuwa ni pamoja na elimu bora na bure kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu.

Vingine ni kuwatoa Watanzania katika lindi la umaskini kwa kuboresha kilimo, viwanda, ujenzi wa reli na barabara na miundo mbinu mingine kama ya afya, mawasiliano na biashara.

Lowassa aliahidi kuwa serikali yake itakuwa rafiki wa watu wa hali ya chini ili kuwainua wamachinga, mama ntilie, bodaboda na wachimbaji wadogowadogo.

Akiwa Viwanja vya Jangwani, leo Lowassa na viongozi wengine waandamizi wa Ukawa watahitimisha kampeni zao kuwaomba wapiga kura wamchague Lowassa na wagombea wengine wote wa Ukawa.

Leave A Reply