The House of Favourite Newspapers

Uchaguzi Simba SC, vigogo kujadiliwa saa 48

BAADA ya zoezi la urudishaji fomu kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Simba kukamilika, kamati ya uchaguzi itatumia siku mbili, sawa na saa 48, kuwajadili wagombea 21 ambao wanahitaji kupata nafasi za uongozi katika timu ya Simba.

 

Simba inatarajiwa kufanya uchaguzi mkuu,Novemba 3, mwaka huu kwa kuchagua viongozi wa nafasi ya mwenyekiti na wajumbe, zoezi hili mwanzo lilianza kusuasua kutokana na kigezo cha mgombea wa uenyekiti kuwa na elimu ya kiwango cha digrii, hali iliyosababisha kuwa na wagombea wawili tu kwa nafasi hiyo ambao ni Sued Nkwabi na Mtemi Ramadhani huku wajumbe 19 wakiwa wamechukua fomu.

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba, Boniface Lihamwike, alisema kuwa kwa sasa zoezi linaendelea vizuri kwa kuwa tayari wagombea wote wamesharejesha fomu na kilichobaki ni kwa kamati kukaa chini na kuanza kujadili majina ya wagombea.

 

“Kila kitu kwa sasa kinakwenda sawa na tunatarajia kamati kukaa siku mbili kuanzia leo (jana) katika Hoteli ya Serena ili kuweza

kuwajadili wagombea kwa kuangalia kama wamekidhi vigezo vya kugombea kama ambavyo walitangaziwa kwa kuangalia nyaraka muhimu ambazo wameambatanisha kwenye fomu.

 

“Baada ya kuweza kuzipitia nyaraka zao, kamati itatoa muda wa kuruhusu pingamizi pamoja na rufaa kwa wagombea na kwa yule ambaye analeta pingamizi, ni lazima aje na mgombea ambaye anamuwekea pingamizi kama ikitokea hajaja na mgombea basi pingamizi linaondolewa kisha tutatangaza utaratibu kwa ajili ya kampeni kisha tumalize zoezi la uchaguzi,” alisema Lihamwike.

 

Lunyamadzo Mlyuka, Dar es Salaam

Comments are closed.