The House of Favourite Newspapers

Uchaguzi Zanzibar umefanyika je, ni mwisho wa matatizo?

0

151025111302_tanzania_woman_zanzibar_512x288_bbc - CopyBILA shaka Mungu ni mwema na tumshukuru kwa kutufikisha leo. Baada ya kusema hayo acha nizungumzie uchaguzi wa marudio uliofanyika juzi Zanzibar.

Swali ambalo watu wengi wanajiuliza, je uchaguzi huo wa marudio utamaliza mgogoro wa kisiasa visiwani?

Wapo walioshauri tofauti na serikali ilivyoamua, kwa mfano Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe aliwahi kushauri kuundwa kwa serikali ya mpito na akatoa wito kwa Rais Dk. John Magufuli kusimamia mchakato wa kuiunda akasema akifanya hivyo kwa nia njema ataweza kuumaliza kabisa mgogoro wa kisiasa visiwani humo.

“Rais Magufuli ndiye Mkuu wa Nchi, kwa mazingira ya dharura ndiye peke yake anaweza kuisimamisha Katiba ya Zanzibar, mamlaka haya hayako kwa mtu mwingine,” alisema.
Alifafanua kuwa rais anayo nafasi kubwa kuingilia kati na kumaliza mgogoro huo kwa kuwa pande zote zinazosigana katika mgogoro huo bado zina imani naye.

Lakini uchaguzi wa marudio umefanyika Jumapili iliyopita na Chama Cha Wananchi (CUF) waliususia kwa madai kwamba ule wa awali ulikuwa huru na haki, wakataka mshindi atangazwe.
Baadaye Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamadi alitoa taarifa akisema hali ilipofikia, inabidi Rais Magufuli aongoze juhudi za kuleta muafaka katika mgogoro huo.
Mapendekezo yote hayo yalipuuzwa.

Katika andiko lake, The Zanzibar Conflict: A Search for Durable Solutions, Professa Gaundence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema kuwa suluhisho la kudumu la mgogoro wa Zanzibar linapaswa kushughulikiwa katika ngazi ya chini na ya juu (micro and macro levels) na kuchukua hatua za kujenga jamii ya kidemokrasia iliyoendelea.

“Katika ngazi ya chini Muafaka I na II lazima utekelezwe pamoja na mapendekezo mengine. Wadau wengi wanaona muafaka II umetekelezwa kikamilifu, lakini hiyo haitoshi kuhakikisha suluhisho la kudumu kwa mgogoro wa Zanzibar na kujenga amani ya kudumu.

Hii ni kwa sababu muafaka huo ulijikita katika masuala ya uchaguzi zaidi. Jamii ya Zanzibar lazima itazamwe kwa uhalisia na kwa upana zaidi. Suluhisho lazima litazamwe kuhusisha masuala kama Muungano, uongozi, utawala wa sheria, elimu, ikiwemo ya uraia na hali ya maendeleo ya kiuchumi,” inasema sehemu ya andiko hilo.

Uchaguzi umefanyika naamini ni suluhisho la muda tu kwa kuwa litakuwa ni la wanasiasa kama ambavyo imezoeleka, lakini suluhu ya kudumu ya matatizo ya Zanzibar ni kutafuta suluhisho la jamii ya Wazanzibari.

Uchaguzi huu uliofanyika uwe kama dira ya kuielekeza nchi katika suluhisho la kudumu ambalo litapatikana kwa wanasiasa wanaokubalika na jamii kukaa na kuweka njia sahihi ya kuafikiana kwa masilahi ya nchi na si ya mtu binafsi mmojammoja, bila kufanya hivyo tutakuwa tunairudisha nchi nyuma kwani kwenye malumbano, hakuna maendeleo.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

Leave A Reply