The House of Favourite Newspapers

Uchumba wa MC Pilipili wapumulia mashine

DAR ES SALAAM: Mambo yamekuwa mambo! Wakati tukijiandaa kwa mnuso kabambe wa ndoa takatifu kati ya wapendanao, Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’ na Phelomena Thadey ‘Cute Mena’, ghafla tu, imeelezwa kwamba uchumba huo unapumulia mashine baada ya mchekeshaji huyo maarufu Bongo kueleza foleni ya wanaume wanaomfuatilia mpenzi wake huyo kila kukicha.

 

Katika mahojiano na Gazeti la Ijumaa baada ya kusambaa kwa habari kuwa Cute Mena kwa sasa anatongozwa kupita maelezo mara tu baada ya kuchumbia, MC Pilipili alisema kuwa wanaume wengi wamekuwa wakimsumbua kila kukicha, hali inayomsababishia kukata tamaa.

 

MC Pilipili alisema kama mchumba wake huyo ataingiwa na shetani na kuwakubalia, basi yupo tayari kuachana naye.

“Hawa wanaume walianza kumfuatilia mchumba wangu muda mrefu kabla hata sijaanza kumtangaza kwenye vyombo vya habari, lakini sasa wamezidi baada ya kumvisha pete ya uchumba.

“Pia nimesikia kuna kijana eti yupo kwenye kituo kimoja cha redio (jina kapuni) naye anamfuatilia, nimebaki ninamuangalia tu kwa sababu wanaomfuatilia wapo wengi.

 

“Kuna mwingine yupo Mwanza, mwingine yupo Mwenge, Ubungo, Mlimani City, Sinza, mwingine anatokea kampuni moja hivi ipo Posta, mwingine yupo Usalama wa Taifa na mwingine ni bodaboda sehemu f’lani hivi. Kwa hiyo mwisho wa siku inategemea na yeye mwenyewe kama wakimuingia, akawaelewa, basi nitamuacha aende, ikiwezekana labda hata uchumba pia naweza nikauvunja,” alisema MC Pilipili.

 

Januari 6, mwaka huu, MC Pilipili alimvalisha pete ya uchumba mpenzi wake huyo ambaye hivi karibuni wanatarajia kufunga ndoa takatifu, licha ya kwamba ni watu wanaoonesha kupendana kwa dhati, lakini kumekuwa na changamoto nyingi kati yao huku wengine wakimpongeza kwa kutimiza ahadi na wengine wakimkejeli kuwa kapotea njia, lakini mwisho wa siku Mungu ndiye msemaji wa mwisho.

Gazeti la Ijumaa linawaombea na kuwatakia kila la kheri katika maandalizi ya ndoa yao. –Mhariri.

Stori: MEMORISE RICHARD, IJUMAA

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

Comments are closed.