Ufafanuzi kadi ya Banda watolewa
Beki wa kati wa Simba, Abdi Banda.
Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam
JUMAMOSI iliyopita beki wa kati wa Simba, Abdi Banda alionyeshwa kadi nyekundu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Kadi hiyo ilizua maswali mengi kwa baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwa uwanjani hapo huku baadhi yao wakidai kuwa mchezaji huyo ameonewa na hakustahili kupewa adhabu hiyo.
Hata hivyo, baada ya kelele nyingi za mashabiki hao hatimaye Chama cha Waamuzi Tanzania (Frat), kimeamua kuitolea ufafanuzi kadi hiyo aliyoonyeshwa Banda ambaye alijiunga na Simba akitokea Coastal Union ya Tanga.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwenyeki wa Frat, Nassor Mwalim, alisema kadi hiyo aliyopewa Banda na mwamuzi wa mechi hiyo namba 153, Jonesia Rukyaa kutoka Bukoba, haikuwa na tatizo lolote.
“Jinsi Banda alivyokuwa akicheza siku hiyo alistahili kadi nyekundu kwani alifanya kosa la aina moja mara mbili licha ya kuwa tayari ameonywa kwa mdomo baada ya kupewa kadi ya kwanza ya njano.
“Alimwambia asirudie kufanya faulo kama hiyo tena kwani ni kinyume na taratibu na sheria 17 za soka, endapo atarudia tena basi atamtoa nje kwa kadi nyekundu.
“Hata hivyo, jambo la kushangaza ni baada ya mchezaji huyo kurudia tena kosa kama hilo ndani ya muda mfupi tu licha ya kuwa ameonywa, kwa hali hiyo ilibidi aonyeshwe kadi ya pili ya njano na kisha nyekundu,” alisema Mwalim na kuongeza:
“Kosa alilofanya Banda katika mechi hiyo lilikuwa ni ‘Breaking up promising attack’ ambalo alilifanya mara mbili wakati Donald Ngoma wa Yanga akiwa tayari ameshaangalia golini, kwa kosa kama hilo adhabu yake ni kadi ya njano ama nyekundu.”
Alipoulizwa Rukyaa kuhusiana na suala hilo hakuwa tayari kusema chochote zaidi ya kudai kuwa hana mamlaka ya kuzungumzia mchezo huo katika vyombo vya habari ila kila kitu kipo katika ripoti yake aliyoiwasilisha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).