The House of Favourite Newspapers

Ufundi wa Nabi, Yanga Full Shangwe

0

RASMI Kocha Mkuu wa Yanga, Noureddine Al-Nabi raia wa Tunisia, jana jioni alianza kibarua cha kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC na tayari inaonekana kuna tabasamu kwa watu wa Yanga.

 

Mchezo huo unaotarajiwa kujaa upinzani mkubwa utapigwa keshokutwa Jumapili saa 2:15 usiku kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.Mtunisia huyo anaanza kukinoa kikosi hicho zikiwa zimebakia siku nne sawa na saa 96 katika kuelekea mchezo huo wa pili wa ligi.

 

Kauonyesha kuwa morali imeanza kuwa juu na kujiamini kumerejea kutokana na ufundi wa kocha huyo aliyoanza kuumwaga kwa wachezaji wake, kupitia ukurasa rasmi wa Yanga katika mtandao wao wa Instagram waliandika:

“Kama ilivyoada kwa wananchi hatuna jambo dogo, wikiendi hii ni zamu ya wana lambalamba kupata dozi kama waliyopata mzunguko wa kwanza.”Ikumbukwe kuwa katika mchezo wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Mbagala jijini Dar, Yanga ilifanikiwa kupata ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Deus Kaseke.

 

Akizungumza na Championi Ijumaa, Meneja Mkuu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema kuwa kocha huyo rasmi alianza kibarua cha kukinoa hicho jana saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Avic Town ilipo kambi hiyo.Saleh alisema kuwa kocha huyo ameanza kibarua hicho akiwa na msaidizi wake, Sghir Hammadi aliyetua naye juzi Jumanne.

 

Aliongeza kuwa kocha huyo ataanza kukinoa kikosi hicho wakati timu hiyo ikiwa katika maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya Azam FC ambao muhimu kwao kupata ushindi.

“Maandalizi ya kuelekea mchezo wetu wa ligi dhidi ya Azam yanakwenda vizuri na leo (jana) jioni kocha wetu mpya ataanza rasmi majukumu ya kukinoa kikosi chetu.“Kocha ataanza kibarua hicho hicho baada ya kukamilisha mambo mbalimbali ikiwemo zoezi la kusaini mkataba wa kuifundisha timu yetu,” alisema Saleh.

 

Yanga imekuwa na mwendo wa kusuasua licha ya kuongoza katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, huku ikionekana wamekuwa hawachezi soka la kuvutia ambapo mashabiki wao wamekuwa wakiwapa presha viongozi na benchi la ufundi kabla ya kutua kwa kocha huyo.

STORI: WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Leave A Reply