The House of Favourite Newspapers

UGANDA: MFANYAKAZI AJIRUSHA KUTOKA KWENYE NDEGE

Mfanyakazi wa shirika la ndege la Emirates jana jioni alijirusha kutoka kwenye ndege ya shirika hilo na kuanguka katika uwanja wa ndege wa Entebbe, Kampala nchini Uganda, ambapo alipata majeraha makubwa.

 

Habari za kuaminika zinasema mfanyakazi huyo ambaye ni mwanamke na ambaye bado hajafahamika jina lake, alianguka muda mfupi kabla ya ndege hiyo kuondoka uwanjani hapo saa 9:25. Kutokana na tukio hilo, ndege hiyo ilibidi iondoke saa 10:21.

Taarifa iliyotolewa na mamlaka ya usafiri wa anga (CAA), mfanyakazi huyo anatibiwa mahali ambapo hapajawekwa wazi, na kwamba mfanyakazi huyo aliufungua mlango wa dharura wa ndege hiyo kabla ya kujirusha chini.

 

Ndege hiyo ya Emirates iliyokuwa katika safari namba EK 730 ilikuwa imeshusha abiria uwanjani Entebbe na ilikuwa ikijitayarisha kuelekea Dubai. Chanzo cha tukio hilo hakijafahamika, lakini mashuhuda wamesema huenda mtu huyo alitaka kujiua.

Waliomwona walisema alikuwa amebeba chupa aliyokuwa ameilengesha kwenye kidevu chake kabla ya kuanguka. Watu wengine wamesema walimwona akiwa analumbana na wafanyakazi wenzake wakati wanapanda ndege hiyo.

 

“Magoti yake yalivunjika na mwili ukiwa umejeruhiwa na vipande vya chupa aliyojirusha nayo,” alisema shuhuda mmoja uwanjani hapo. Alipoulizwa kuhusu tukio hilo, Msemaji Mkuu wa CAA, Vianney Luggya, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wangetoa taarifa baadaye.

 

Na Edwin Lindege na Mtandao.

Comments are closed.