Uganda Yafunga Mitandao ya Kijamii Kabla ya Uchaguzi

MAMLAKA ya udhibiti wa mawasiliano nchini Uganda imeamuru kufungwa kwa mitandao ya kijamii na njia za kutumiana ujumbe kabla ya uchaguzi unaofanyika kesho, Alhamisi.

 

Upigaji kura unafanyika baada ya kampeni za umwagaji damu zaidi katika utawala wa Yoweri Museveni akipambana na mpinzani mkuu, mwanamuziki ambaye sasa ni Mbunge, Bobi Wine, ambaye amewavutia vijana wengi ambao kwa muda mrefu walimjua rais mmoja tu — Museveni.

 

Wine, ambaye ametumia muda wake karibu wote wa kampeni akiwa amevaa nguo za kuzuia risasi¬† na kofia za kuzuia mabomu ya machozi, pamoja na kukamatwa kila mara, amewataka wapiga kura “kulinda” kura zao zisiibiwe.

 

Hata hivyo, wachunguzi wengi wanaamini kwamba licha ya umaarufu wake mkubwa, mwanamuziki huyo (38)  hawezi kumshinda Museveni (76) ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986.

 

Watu milioni 18 wamejiandikisha kupiga kura kumchagua rais na wabunge.

 

Katika maandamano ya kupinga utawala wa Museveni yaliyofanyika Novemba 2020, watu 54 waliuawa na majeshi ya usalama.

Toa comment