Uganda Yazidi Kukumbwa na Mlipuko wa Ebola
Idadi ya visa vya Ebola nchini Uganda imeongezeka hadi 14 wiki hii, kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa barani Afrika (Africa CDC). Mlipuko mpya umeibuka kufuatia kifo cha mtoto wa miaka minne, huku maambukizi yakiripotiwa katika wilaya tano kati ya 146, ikiwemo Kampala, ambako mlipuko ulitangazwa rasmi Januari 30.
Taarifa za afya zinaonyesha kuwa visa vitatu kati ya vitano vipya vimethibitishwa kuwa Ebola, huku viwili vikihisiwa kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa ugonjwa huo. Hata hivyo, wataalamu wanasema hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya mlipuko huu mpya na ule wa awali uliokuwa na visa tisa, vikiwemo vifo viwili vilivyothibitishwa.
Wasiwasi umeongezeka kuhusu ukosefu wa uwazi katika utoaji wa taarifa, kwani hospitali kadhaa jijini Kampala zimethibitika kushughulikia wagonjwa wa Ebola bila kutoa taarifa kwa umma. Serikali kupitia Wizara ya Afya inasisitiza kuwa hali iko chini ya udhibiti, ingawa haioni ulazima wa kutoa taarifa kwa kila tukio.
Kwa sasa, hakuna chanjo iliyoidhinishwa kwa aina ya Sudan ya virusi vya Ebola vinavyosambaa Uganda. Ugonjwa huu huenea kupitia majimaji ya mwili wa mgonjwa au vitu vilivyochafuliwa, na dalili zake ni pamoja na homa kali, kutapika, kuhara, maumivu ya misuli, na wakati mwingine kutokwa damu ndani na nje ya mwili. Ugonjwa huo mara nyingi huanza kwa mgonjwa aliyeambukizwa kupitia mnyama au kula nyama yake.