The House of Favourite Newspapers

Ugomvi wa Aboud Jumbe na Nyerere ulivyotetemesha nchi-3

1

majinabcTunaendelea kuchambua ugomvi wa Nyerere na Rais wa Awamu ya Pili wa Zanzibar, Alhaji Aboud Jumbe:

Baadaye Aboud Jumbe Mwinyi akawa kipenzi cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere na Tanzania Bara akapaona kama nyumbani Zanzibar.

Lakini kadiri alivyozidisha ukaribu na Nyerere ndivyo alivyozidi kujitenga na siasa pamoja na mambo mengi ya visiwani.

Baada ya muda mfupi akapaona Dar es Salaam kuwa kwake zaidi kuliko Zanzibar hasa baada ya kujenga Mjimwema, Kigamboni. Akawa anatumia ndege kwenda Zanzibar mchana kufanya kazi na kurejea Dar jioni kulala.

Kwa sababu hii, baadhi ya viongozi Zanzibar wakaanza kumlalamikia na kudai kuwa alikuwa akikwamisha mambo ya kiuongozi visiwani.

Wakati baadhi ya viongozi Visiwani wakimnung’unikia Nyerere alifurahishwa na utendaji wa Jumbe na kuingiwa hamu ya kutaka muungano zaidi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Ndipo akabuni mpango wa kuviunganisha vyama vya siasa, kile cha bara,Tanu na ASP cha Zanzibar.

Muungano kadiri ulivyozidi kuimarika, Alhaji Jumbe akajiona kama atakuwa mrithi halali wa nafasi ya Rais Nyerere.

Alijisahau na ikawa badala ya kushughulikia utawala wa visiwani, akawa muda mwingi yupo Dar na wadadisi wa mambo ya kisiasa wanaamini kwamba matarajio hayo ya kurithi nafasi ya Nyerere yalimfanya akubali kirahisi kuungana kwa ASP na Tanu.

Kuanzia Februari 1972 hadi Aprili 1983,  chini ya utawala wake Jumbe Zanzibar, Nyerere alipendekeza marekebisho zaidi ya kuimarisha muungano ndipo Wazanzibari wakaanza malalamiko kwamba kuna mpango wa ‘kuimeza’ Zanzibar ndani ya muungano.

Hofu ya Wazanzibari iliongezeka pale Watanzania Bara walipopendekeza kuwa na serikali moja ya muungano

badala ya muundo wa serikali mbili. Kelele za Wazanzibar zikaanza.

Hofu hiyo iliwafanya Wazanzibari kumweka pabaya Jumbe ambaye alikuwa kipenzi cha Nyerere; akaanza kuitwa msaliti.

Kuona hivyo, Jumbe aligutuka, akawa njia panda. Ili kurejesha imani ya Wazanzibari, Jumbe aliomba ushauri kutoka kwa makatibu wakuu wote wa wizara na watendaji wakuu wengine wa Serikali ya Zanzibar.

Nini kiliendelea? Fuatilia Jumanne ijayo.

1 Comment
  1. SEIF KIHAMBWE says

    safi kwakujua histor tusioijuwa ila tuendeleze na stor

Leave A Reply