The House of Favourite Newspapers

Ugomvi wa Aboud Jumbe na Nyerere ulivyotetemesha nchi-4

0

Tunaendelea na uchambuzi wa kuhusu ugomvi wa Aboud Jumbe na Mwalimu Julius Nyerere kuhusu Muungano, endelea:

Makatibu wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) waliomshauri Jumbe akiwa rais, wote walikataa muundo wa Muungano wenye serikali moja, wakapendekeza kuwe na serikali tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano tu.

Mwaka 1983, Edward Moringe Sokoine, aliteuliwa kuwa waziri mkuu. Sokoine alikuwa kiongozi makini, shupavu, mnyoofu na mwenye mvuto mkubwa kwa watu.

 Na katika kipindi kifupi tu, alijidhihirisha kuwa chaguo la watu na mrithi wa Mwalimu Nyerere ambaye naye alimkubali kwa utendaji wake wa kazi na kuwa adui wa rushwa.

Mwalimu Nyerere akawa anaonesha upendeleo dhahiri kwa Sokoine kuliko kwa Jumbe kutokana na sababu kuu tatu:

Moja ni kwamba, Mwalimu Nyerere alianza kumwona Jumbe kuwa ni mtu asiyeungwa mkono na watu wa chini (umma) Visiwani. Alimwona pia kama dikteta mkimya, asiyeweza kushauriwa akashaurika na watu wa chini yake.

Mwalimu Nyerere alimgutukia Jumbe kuwa alikuwa na tamaa ya madaraka hasa kwa kutaka kumrithi nafasi ya rais.

Jumbe kuona hivyo, alianza kuwa mtu wa dini na alizuru nchi nzima akitoa mihadhara kwenye misikiti na Mwalimu Nyerere ikamlazimu atoe waraka maalum wa rais (Presidential Circular), kuwakumbusha viongozi wa kitaifa kutojitambulisha na kuiingiza serikali katika mambo ya kidini.

 Hata hivyo, Jumbe alipuuza waraka huo, akaendelea na harakati zake.

Habari zikamfikia Jumbe juu ya chuki za Mwalimu dhidi yake, akaumia! Zikamvunja moyo; uhasama kati ya Jumbe na Nyerere ukawa mkubwa. Katika hali hiyo Muungano ukaanza kutikiswa.

Hatua ya kwanza iliyoanza kutikisa Muungano ilikuwa ni kumrejesha Tanzania Bara, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Damian Lubuva (ambaye sasa ni Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi); badala yake akamteua raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy na kumpa uraia kushika wadhifa huo.

Usikose kusoma muendelezo wa makala haya wiki ijayo.

Leave A Reply