The House of Favourite Newspapers

Ugomvi wa Aboud Jumbe na Nyerere ulivyotetemesha nchi-5

0

majinabc

Na Elvan Stambuli

Kama nilivyosema wiki iliyopita, hatua ya kwanza iliyoanza kutikisa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ilikuwa ni pale Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Jaji Damian Lubuva aliporejeshwa Tanzania Bara na badala yake Rais Aboud Jumbe akateua raia wa Ghana, Alhaj Bashir K. Swanzy na kumpa uraia kushika wadhifa huo, Endelea…
Kuanzia hapo, madai ya Wazanzibari kutaka mabadiliko ya Katiba, kupitia mihadhara, magazeti na redio yalipamba moto.
Kukaanzishwa ‘redio pori,’ wengi watakumbuka matangazo ya redio hiyo ya mafichoni ambayo ilipachikwa jina la KIROBOTO TAPES ya kudai Wazanzibari warejeshewe visiwa vyao.
Ni mashushushu wa kijeshi wa bara ndiyo waliogundua baadaye kuwa ipo msituni, ikazimwa, sikumbuki kama kuna watu walifikishwa mahakamani kwa kumiliki redio hiyo.
Kwa kupitia Mghana, Jaji Bashir Swanzy, Serikali ya Jumbe iliandaa hati ya mashtaka kuhoji muundo na uhalali wa Muungano kwenye Mahakama Maalum ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo kazi yake pekee, kwa mujibu wa ibara ya 126 ya Katiba ya Muungano ya 1977, “ni kusikiliza shauri lililoletwa mbele yake na kutoa usuluhishi juu ya suala lolote linalohusika na tafsiri ya Katiba, iwapo tafsiri hiyo au utekelezaji wake unabishaniwa kati ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.”
Hati hiyo ya mashtaka ‘ilipotea’ mezani kwa Rais Aboud Jumbe katika mazingira ya kutatanisha sana na kuibukia mikononi mwa Mwalimu Nyerere Msasani Dar!
Taarifa za uhakika zinaonesha kuwa waliofanikisha kazi ya kuiba hati hiyo na kuipeleka kwa Mwalimu Nyerere ni baadhi ya vigogo ambao sasa wako katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa, wakati ule wakiwa SMZ.
Haraka Mwalimu Nyerere aliitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec) mjini Dodoma, Januari 1984 na Rais Aboud Jumbe akabanwa kwa madai ya kutaka kuuvunja Muungano kwa kuuhoji.
Nchi ikatangaziwa kwamba kuna “kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar.”
Alihojiwa na Nec na bila kumung’unya maneno, Jumbe alikiri kuandaa hati hiyo kama moja ya haki zake za kikatiba, jambo ambalo lilizidi kumtibua Mwalimu Nyerere.
Usikose kusoma muendelezo wa makala haya wiki ijayo.

Leave A Reply