The House of Favourite Newspapers

Ugomvi Wa Ndoa Wasababisha Nyumba 300 Kuungua Kenya

 

KWA mujibu wa tovuti ya gazeti la Star la nchini Kenya, ugomvi wa wanandoa uliotokea Jumanne usiku ulianza kwa maneno na kisha kuvaana mwilini, na katika purukushani hizo, jiko lao la gesi likadondoka na kulipuka.

 

Moto ukatanda ndani ya nyumba, na baada ya muda mfupi ukazikumba nyumba nyengine pia.    Eneo ulipozuka moto huo ni kitongoji maarufu cha Kibera jijini Nairobi ambacho wakaazi wake ni maskini.

 

Makazi katika eneo hilo hayajapangiliwa na nyumba zimekaribiana mno, hivyo linapotokea janga la moto, ni kawaida kwa zaidi ya nyumba moja kuathirika.

 

Hata hivyo, si jambo la kawaida kwa moto kuunguza nyumba mpaka 300, na kuacha maelfu ya wakazi bila makao. Mamlaka zimeamua kuficha utambulisho wa wanandoa hao kwa makusudi ili kuwalinda dhidi ya ghadabu ya wakazi wengine ambao wamethirika pakubwa.

 

 

Eneo lilitokea moto huo linaitwa Laini Saba na tayari mwakilishi wake kwenye bunge la Kaunti ya Nairobi, Cecilia Ayot, amesema mvua zimefanya hali izidi kuwa mbaya.

 

“Watu wameachwa bila makazi. Bahati mbaya zaidi ni kuwa kwa mvua zinazoendelea, hata ile sehemu ambayo walikuwa wanajihifadhi haipo tena,” amesema Ayot.

 

Mwakilishi huyo pia amekemea vikali ukatili wa majumbani na ugomvi: “Kuna namna nyingi za kutatua matatizo, na ugomvi si njia muafaka ya kufanya hivyo. Watu (wanaogombana) inawapasa waombe ushauri na usuluhishi badala ya kupigana; tumeona madhara ya ugomvi na jinsi ulivyoathiri maisha ya maelfu ya watu kwa kuteketeza nyumba 300.”

 

Kikosi cha zimamoto cha jiji la Nairobi kimejitetea kuwa ujenzi wa kiholela katika eneo hilo uliwazuia kulifikia eneo hilo na kuuzima moto kwa haraka.

Comments are closed.