The House of Favourite Newspapers

Ugonjwa sugu wa figo (Chronic Kidney Disease)

0

Chronic_kidney_disease_4062991_i0Leo tunajadili ugonjwa sugu wa figo au Chronic Kidney Disease kwa kitabibu. Ugonjwa huu hutokea pale figo zinapopoteza uwezo wa kutenda kazi ambayo hutokea taratibu na huchukua muda wa takriban miezi kadhaa hata miaka.

Figo zinapopoteza uwezo wake wa kutenda kazi, kusanyiko na limbikizo la maji, uchafu na sumu hutokea mwilini mwa mgonjwa na pia husababisha kutokea kwa maradhi mengine.
Hatua za ugonjwa sugu wa figo

Ugonjwa sugu wa figo umegawanywa katika hatua kuu tano, kulingana na ukubwa wa tatizo. Hatua hizo zimegawanywa kulingana na kiwango cha Glomerular Filtration Rate kwa kifupi GFR- ni kiwango kinachoonesha uwezo wa utendaji kazi wa figo.

GFR hupima uwezo wa glomeruli au chujio la figo katika kuchuja uchafu, maji pamoja na sumu nyingine kwa kila dakika moja kwa mtu mwenye wastani wa urefu wa mita mraba 1.73. Kadiri GFR inavyopungua ndivyo inavyoashiria ukubwa wa tatizo katika figo.

Hatua ya kwanza mgonjwa huwa na GFR ya zaidi ya mililita 90 kwa dakika kwa mita mraba 1.73, ambapo madhara madogo huwepo katika figo, huku kiungo hicho kikiendelea kuchuja uchafu kama kawaida.

Hatua ya pili ni pale GFR inapokuwa ya kati ya mililita 60-89 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 na katika hatua hii, kiwango cha utendaji kazi cha figo hushuka kwa kiasi kidogo.

Hatua ya tatu, GFR huwa kati ya mililita 30-59 kwa dakika kwa mita mraba 1.73. Katika hatua hii utendaji kazi wa figo hupungua zaidi, wakati katika hatua ya nne GFR hushuka zaidi na kuwa kati ya mililita 15-29 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 na hapa utendaji kazi wa figo huwa wa chini mno.

Katika hatua ya tano mgonjwa huwa na GFR chini ya mililita 15 kwa dakika kwa mita mraba 1.73 hatua ambayo huitwa pia kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo au CRF neno ambalo tutalitumia zaidi kumaanisha kushindwa kufanya kazi sugu kwa figo yaani Chronic Renal Failure.

Ugonjwa sugu wa figo ni maarufu zaidi miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Kwa mujibu wa ripoti ya kituo cha udhibiti wa magonjwa cha nchini Marekani (CDC), ugonjwa sugu wa figo ni miongoni mwa matatizo ya kiafya yanayojitokeza kuchukua chati za juu sana nchini humo.

Mambo kadhaa yanahusishwa na ongezeko la ugonjwa sugu wa figo, miongoni mwayo ni ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu, unene na uzee. Aidha, mabadiliko katika tabia na namna watu wanavyoishi pia vimeonekana kuchangia ongezeko hili kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na kwamba ugonjwa sugu wa figo hutokana na magonjwa kadhaa ambayo kimsingi yanaathiri figo yenyewe, visababishi vikuu vya ugonjwa sugu wa figo ni kisukari na shinikizo la damu.

Leave A Reply