The House of Favourite Newspapers

Ugonjwa wa Figo Unaohusiana na Ukimwi

KUNA matatizo mengi ambayo hukumbana nayo wagonjwa wa Ukimwi duniani kote. Figo (kidney) ni moja ya kiungo muhimu cha kuchuja sumu mwilini. 

 

Wagonjwa hawa huathiriwa sana na ugonjwa wa figo. Ugonjwa wa figo unaohusiana na Ukimwi kitaalamu HIV-Associated Nephropathy au kwa kifupi HIVAN, unaweza kusababishwa na mashambulizi ya moja kwa moja ya Virusi Vya Ukimwi kifupi VVU kwenye figo au madhara yanayotokana na matumizi ya madawa ya kurefusha maisha (ARVs).

 

Ni wazi kwamba wagonjwa wengi wa Ukimwi wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya figo kwa sababu ya kupungukiwa na maji mwilini kutokana na kutapika mara kwa mara, kupoteza chumvi mwilini, au lishe duni.

 

Zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa walioandikishwa kuanza ARVs hospitalini huwa wana matatizo ya figo yaliyotokana na VVU ambapo huwaathiri zaidi wanawake kuliko wanaume, wenye uzito mdogo na wale waliokuwa na CD4 chini ya 200.

 

Watafiti wameonesha uhusiano wa mashambulizi ya moja kwa moja ya VVU- 1 kwenye figo. Pia kuna uhusiano mkubwa wa vinasaba na vyanzo vya kimazingira vinavyochochea kutokea kwa tatizo hili kwa watu.

VVU-1 hushambulia zaidi chujio za figo (glomeruli) pamoja na seli za kuta za mirija yake kuliko sehemu nyingine yeyote ya figo.

 

Hali hii husababisha kuharibika kwa chujio za figo pamoja na mirija na kufanya kazi ya uchujaji uchafu pamoja na utengenezaji wa mkojo kuvurugika. Matokeo yake mkojo huwa na kiwango kingi cha protini kuliko kawaida, chujio huwa na makovu hali kadhalika nayo mirija (tubulointerstitial scarring).

 

DALILI

Pamoja na kuwa na dalili zote za magonjwa ya wagonjwa wa HIVAN huwa pia na tabia/ dalili zifuatazo: Muonekano wa mgonjwa hupoteza kiwango kingi cha protein katika mkojo kwa siku. Hupoteza pia kiwango kingi cha albumin (aina nyingine muhimu sana ya protini).

 

Aidha, huwa na kiwango kingi cha mafuta mwilini pamoja na kupoteza sana protini, wagonjwa wengi wa HIVAN hawana hali ya kuvimba miguu (edema).

 

Huwa na shinikizo la damu la kawaida na mrundikano usiyo wa kawaida wa urea au mazao mengine machafu yanayotokana na Nitrogen katika damu. Muonekano wa figo katika Ultrasound au CT scan huwa na figo zilizo na ukubwa wa kawaida au zilizovimba sana (kubwa kuliko kawaida).

 

Muonekano wa figo katika biopsy: Figo huwa na makovu makovu katika chujio zake yanayoonekana katika darubini tu. Pia kiwango cha CD4+ T-cells cha mgonjwa: Kwa kawaida kiwango cha seli za CD4+ kwa wagonjwa wenye HIVAN huwa chini ya 200 cells/μL.

 

Hata hivyo, HIVAN inaweza kutokea hata kwa mgonjwa mwenye kiwango cha juu cha CD4. Wagonjwa wenye CD4 chini ya 50 cells/ μL wana hatari zaidi ya kufa mapema kutokana na HIVAN.

Vipimo na uchunguzi

Kuna vipimo vingi kama vile cha mkojo (urinalysis), vipimo vya utendaji kazi wa figo (renal function tests), vipimo vya kuchunguza uwiano wa madini mwilini (electrolytes analysis) FBP kwa ajili ya kuchunguza wingi wa damu, kiwango cha seli mbalimbali za damu na uwepo wa magonjwa mengine yanayomuathiri mgonjwa.

 

Pia kuna kipimo cha Renal Biopsy; madaktari wengi hupenda kufanya biopsy kwa wagonjwa wanaopoteza zaidi ya gramu 1 ya protini kwa siku kupitia kwenye mkojo. Kuna vipimo vya Ultrasound ya figo, mirija pamoja na kibofu cha mkojo, CT ya figo, kiwango cha CD4 pamoja na wingi wa VVU (viral load).

 

MATIBABU

Matibabu ya HIVAN yanajumuisha matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs) kwa wale ambao bado hawajaanza kutumia dawa hizo, kurekebisha au kubadilisha aina ya dawa za ARVs kwa wale ambao tayari wamekwisha anza kutumia ili zisimdhuru mtumiaji, na matumizi ya dawa nyingine kama atakavyoelekeza daktari.

Comments are closed.