The House of Favourite Newspapers

UGONJWA WA FIGO UNAOHUSIANA NA UKIMWI

WAGONJWA wa Ukimwi huathiriwa pia figo. Ugonjwa wa figo unaohusiana na Ukimwi (HIV-Associated Nephropathy au kwa kifupi HIVAN) unaweza kusababishwa na mashambulizi ya moja kwa moja ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kwenye figo au madhara yanayotokana na matumizi ya madawa ya kurefusha maisha (ARVs). 

 

Wagonjwa wengi wa Ukimwi wapo katika hatari ya kupata magonjwa ya figo kwa sababu ya kupungukiwa na maji mwilini kutokana na kutapika mara kwa mara, kupoteza chumvi mwilini, au lishe duni.

 

Wanaume huathirika zaidi kuliko wanawake katika uwiano wa 10 kwa moja wakati wastani wa umri wa watu wenye HIVAN ni miaka 33 ingawa HIVAN huwapata pia watoto. Kuna uhusiano mkubwa wa vinasaba na vyanzo vya kimazingira vinavyochochea kutokea kwa tatizo hili. VVU-1 hushambulia zaidi chujio pamoja na seli za kuta za mirija yake kuliko sehemu nyingine yoyote ya figo.

 

Hali hii husababisha kuharibika kwa chujio pamoja na mirija na kufanya kazi ya uchujaji uchafu pamoja na utengenezaji wa mkojo kuvurugika. Matokeo yake mkojo huwa na kiwango kingi cha protini kuliko kawaida, chujio huwa na makovu hali kadhalika nayo mirija.

 

Pamoja na kuwa na dalili zote za magonjwa ya figo, dalili zifuatazo huonekana kwa kuangalia muonekano wa mgonjwa kwani hupoteza kiwango kingi cha protein katika mkojo (zaidi ya gramu 3.5 kwa siku). Hupoteza pia kiwango kingi cha albumin (aina nyingine muhimu sana ya protini).

 

Aidha huwa na kiwango kingi cha mafuta mwilini. Pamoja na kupoteza sana proteini, wagonjwa wengi wa HIVAN hawana hali ya kuvimba miguu. Huwa na shinikizo la damu na mrundikano usio wa kawaida wa urea au mazao mengine machafu yanayotokana na Nitrogen katika damu.

 

Muonekano wa figo katika Ultrasound au CT scan: Wagonjwa wenye HIVAN huwa na figo zilizo na ukubwa wa kawaida au zilizovimba sana (kubwa kuliko kawaida). Muonekano wa figo katika biopsy: Figo huwa na makovu makovu katika chujio zake yanayoonekana katika darubini tu.

 

Vipimo na uchunguzi

Kipimo cha mkojo (urinalysis): Pamoja na kuonesha kiwango cha juu cha protini katika mkojo, kipimo hiki pia huonesha damu katika mkojo, chembe nyeupe za damu, vipande vidogo vinavyojulikana kama casts pamoja na chembechembe za mafuta.

Vipimo vya utendaji kazi wa figo; Vipimo vya kuchunguza uwiano wa madini mwilini (electrolytes analysis): Kwa sababu ya mrundikano wa maji mwilini, wagonjwa wenye HIVAN huwa na upungufu wa madini ya sodiam (hyponatremia) na ongezeko la madini ya potassium.

 

Hali hii ni hatari kwa utendaji kazi wa viungo vya mwili hususan moyo kwa vile inaweza kusababisha shambulio la ghafla la moyo na hatimaye kifo kwa mgonjwa. Ultrasound ya figo, mirija pamoja na kibofu cha mkojo, CT ya figo, kiwango cha CD4 pamoja na wingi wa VVU (viral load). Kuna viwango vingi tu vya tatizo hili.

TIBA YAKE

Matibabu ya HIVAN yanajumuisha matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs) kwa wale ambao bado hawajaanza kutumia dawa hizo, kurekebisha au kubadilisha aina ya dawa za ARVs kwa wale ambao tayari wamekwisha anza kutumia ili zisimdhuru mtumiaji na matumizi ya dawa nyingine kama inavyoelezwa hapa chini.

 

Baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa matumizi ya dawa ya Captopri kwa wagonjwa wa figo husaidia kuongeza muda wa figo kufanya kazi kwa wastani wa kati ya mwezi mmoja mpaka sita (6), wakati dawa ya fosinopril ilisaidia kuongeza muda wa kufanya kazi wa figo kwa wastani wa miezi 16.

Comments are closed.