The House of Favourite Newspapers

UGONJWA WA KUHARISHA KWA MTOTO -2

Wiki iliyopita tuliwaeleza kirefu kuhusu ugonjwa wa kuhara kwa watoto, leo tunamalizia makala hayo kwa kueleza dalili zake na matibabu yake, ni vema kujua hayo kwa usalama wa watoto wetu, endelea:

 

DALILI

WATOTO wanaohara kwa sababu ya rotavirus huwa na dalili kuu tatu ambazo ni homa, kutapika na kuharisha. Kawaida choo kinakuwa cha majimaji sana.

 

Wakati mwingine kuharisha kunaweza kujitokeza baadaye baada ya kutapika au homa. Joto la mtoto huwa si kali sana ingawa baadhi ya watoto wanaweza kuwa na joto kali linalozidi nyuzi joto 39 za sentigradi. Kutapika kunaweza kusiwe zaidi ya saa 24. Vilevile wanaweza kuwa na kuchefuchefu, maumivu ya tumbo, kulia pasipo kutulia akibembelezwa na uchovu.

 

Vifo husababishwa na upungufu wa maji mwilini. Upungufu wa maji waweza kuambatana na upungufu na kukosekana uwiano wa madini mwilini. Aidha kunaweza kusababisha madhara katika figo na katika mfumo wa neva na kusababisha mtoto kupoteza fahamu, kuwa na mapigo ya moyo ya kasi, kushindwa kula na kunywa, kuwa na macho yaliyolegea na kuingia ndani sana, kushindwa kutoa mkojo kabisa, kutotoa machozi na mdomo kuwa mkavu sana.

 

Unapoona dalili hizi wakati mtoto wako anaharisha unapaswa kumpeleka haraka kituo cha afya ili kupata ushauri wa wataalamu wa afya.

MATIBABU

Ingawa yawezekana mtoto kupona bila hata matibabu lakini ni jambo muhimu kuchunguza madhara yanayoweza kusababishwa na upungufu wa maji mwilini, hivyo basi msingi wa matibabu ni kurudisha kiasi cha maji kilichopotea.

 

ORS ambayo ni mchanganyiko wenye uwiano mzuri wa chumvi na sukari ni aina ya tiba inayopendekezwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya matibabu. Uwiano uliopo katika ORS huwezesha utumbo wa mtoto kufyonza vizuri maji na madini mengine.

 

Matibabu ya kuharisha kwa watoto yanaweza kugawanywa katika awamu kuu mbili, Mosi kurudisha maji yaliyopotea na pili kuendelea kuupa mwili maji kwa ajili ya mahitaji ya kila siku. Kwa vile chanzo kikuu cha kuhara kwa watoto ni maambukizi ya virusi, haishauriwi kutumia dawa za kuua bakteria yaani antibiotics kama sehemu ya matibabu.

 

Hata hivyo, antibiotics zinaweza kutumika tu pale ambapo itathibitika kuwa kuharisha kumesababishwa na bakteria na anayethibitisha ni daktari.

Comments are closed.