The House of Favourite Newspapers

UGONJWA WA KUHARISHA KWA MTOTO

KUHARISHA kwa watoto ni tatizo linaloshika nafasi ya pili duniani kwa kusababisha vifo miongoni mwa watoto chini ya miaka mitano. Kuharisha huelezwa kuwa ni upotevu wa maji na madini muhimu kwa mwili wa binadamu (electrolytes) kupitia kinyesi na kupelekea upungufu wa maji mwilini.  

 

Kuharisha kunasababishwa na aina mbalimbali za vimelea ingawa pia kunaweza kusitokane na maambukizi ya vimelea (non-infectious causes). Vimelea vinavyosababisha kuharisha ni:

VIRUSI: Virusi vinaongoza katika kusababisha tatizo la kuharisha kwa watoto katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.

 

Bakteria: Wanasababisha kuharisha kwa asilimia chache 2-10. Kuharisha kunakosababishwa na bakteria husababisha upotevu mdogo wa maji ikilinganishwa na Virusi mfano wa bakteria wanaoweza kusababisha tatizo hili ni Campylobacter, Salmonella, Shigella, na Escherichia coli.

 

Parasite pia husababisha kuhara, lakini aina hii ya kuhara huwa ni sugu zaidi (chronic diarrhea) kwa ujumla na mara nyingi haambatana na homa, kutapika na upungufu wa maji mwilini. Giardia lamblia na Cryptosporidium parvum ni moja ya aina hii za parasite wanaosababisha kuhara.

 

Sababu ambazo hazihusiani na maambukizi ya vimelea yaani non infectious causes ni pamoja na kula chakula kilichochanganywa na sumu au kumeza sumu, matatizo katika sehemu ya utumbo mwembamba na mnene na matatizo ya usagaji chakula. Kwa vile sababu kuu ya kuharisha ni kutokana na virusi, tutazungumzia aina kuu ya virusi wanaosababisha kuhara.

 

Kuna aina takribani 4 za virusi wanaojulikana ambao ni Rotavirus, Adenovirus, astrovirus na norovirus. Kati ya hivi jamii ya Rotavirus ndio wanaongoza duniani kote katika kueneza na kusababi sha kuharisha kwa watoto wachanga na wadogo na ndiyo chanzo kikuu cha vifo vinavyotokana na kuhara miongoni mwa watoto chini ya umri wa miaka 5.

Hatari zaidi ni kwa wale watoto walio na uzito wa kuzaliwa chini ya gramu 1500, vilevile uzito kati ya gramu 1500-2499. Ukali wa ugonjwa ni mkubwa zaidi kwa watoto wenye umri wa miezi 3-24.

 

Watoto wachanga chini ya miezi 3 wanapata sehemu ya kinga (antibodies) kutoka kwa mama anayenyonyesha na vilevile kinga mtoto aipatayo kupitia kondo la nyuma (placenta) kabla ya kuzaliwa. Kwa maana hiyo basi shambulizi la awali baada ya miezi 3 lina uwezekano wa kusababisha ugonjwa mkali zaidi.

 

Jamii hii ya Virusi wana uwezo wa kuenea kwa urahisi sana toka kwa mtoto mmoja kwenda kwa mwingine. Kimsingi wanaenea kwa njia ya kinyesi. Ni rahisi mtoto kupata uambukizi wa rotavirus iwapo atakula chembechembe za kinyesi zenye vimelea hivi.

 

Mtu mwenye vimelea hivi anaweza kuambukiza mtu mwingine hata kabla dalili hazijaanza kujionesha kwake au hata siku kadhaa baada ya dalili kujionesha.

Itaendelea wiki ijayo

Comments are closed.