UGONJWA WA KUUMWA VIUNGO VYA MWILI (ARTHRITIS)

UGONJWA wa maumivu ya viungo huitwa kwa jina lingine yabisikavu. Jina la Kingereza la ugonjwa huo, ‘arthritis, linatokana na maneno ya Kigiriki yanayomaanisha viungo vilivyovimba.  Mbali na kuathiri viungo, magonjwa hayo yanaweza kuathiri pia misuli, mifupa, na mishipa inayounganisha misuli na mifupa mbalimbali inayogandamiza viungo.Aina fulani za yabisikavu zinaweza kuathiri ngozi yako, maungo ya ndani ya mwili, na hata macho yako. Tutachunguza hasa magonjwa mawili ya aina ya yabisikavu, yaliyo ya kawaida sana—ugonjwa wa osteoarthritis na baridiyabisi.

Kiungo ni mahali ambapo mifupa miwili imeunganishwa. Mfuko unaonyumbuka hufunika viungo fulani vinavyolainishwa na umajimaji mzito.Mfuko huo huvilinda viungo hivyo na kuvitegandamiza na una utando wa ndani unaotoa umajimaji huo wenye kulainisha.

Ncha ya mifupa iliyomo ndani ya mfuko huo imefunikwa kwa mfupa mwororo unaoitwa gegedu ambayo inazuia mifupa yako isisuguane. Nayo hulinda viungo vyako kwa kupunguza shinikizo na kwa kufanya mifupa yote ihimili shinikizo kwa usawa. Kwa mfano, unapotembea, kukimbia, au kuruka, shinikizo kwenye viuno na magoti yako linaweza kuwa mara nne hadi mara nane ya shinikizo la uzito wako, gegedu husaidia mifupa yako kuhimili uzito huo inaposhinikizwa.

Mtu anaposhikwa na ugonjwa wa baridi yabisi, mfumo wa kinga wa mwili huanza kushambulia viungo vyake. Kwa sababu isiyojulikana, chembe nyingi za damu, ambazo ni chembe muhimu katika mfumo wa kinga wa mwili huingia ghafla katika vitundu vya kiungo. Jambo hilo husababisha utendaji mwingi wa kemikali ambao hufanya kiungo kifure.

Huenda chembe zinazotokeza umajimaji zianze kuongezeka kwa wingi sana, na kusababisha uvimbe unaoitwa pannus. Kisha uvimbe huo hutokeza vimeng’enya vinavyoharibu gegedu. Sasa kwa sababu mifupa inaweza kugusana, inakuwa vigumu kusogeza kiungo na hiyo husababisha maumivu makali sana. Misuli pia hupoteza nguvu. Hiyo inafanya kiungo kianze kulegea na kuteguka kwa kadiri fulani, na mara nyingi kuharibika umbo.

Kwa kawaida ugonjwa wa baridiyabisi huathiri viwiko, magoti, na miguu kwa wakati mmoja.Asilimia 50 ya wagonjwa wanaougua baridiyabisi hupata pia uvimbe au vinundu chini ya ngozi. Wengine wana upungufu wa damu, na wanaumwa na koo na macho makavu. Uchovu na dalili za mafua, kama vile homa na maumivu ya misuli, ni dalili nyingine za baridiyabisi.

Si wagonjwa wote wanaougua baridiyabisi walio na dalili zilezile, na hata muda ambao wagonjwa huugua hutofautiana. Huenda mtu mmoja akaanza kuumwa na kukakamaa polepole kwa muda wa majuma kadhaa au hata miaka. Baadhi ya watu huugua baridiyabisi kwa muda wa miezi michache tu kisha wanapona kabisa, wengine wanaugua kwa miaka mingi.

Wanaopatwa na maradhi haya hasa ni wanawake wa makamo. Hata hivyo, mtu yeyote wa umri wowote ule, watoto, na vilevile wanaume, wanaweza kupata ugonjwa huo. Wale walio na watu wa ukoo wenye baridiyabisi, wanakabiliana na hatari ya kuupata kuliko watu wengine.

Uchunguzi mbalimbali unaonyesha kwamba kuvuta sigara, kunenepa kupita kiasi, na kutiwa damu mishipani huzidisha hatari ya kupatwa na ugonjwa huo. Ugonjwa wa osteoarthritis hutofautiana na baridiyabisi kwa kuwa hauenei hadi sehemu nyingine za mwili bali huathiri kiungo kimoja tu au viungo vichache. Gegedu inapoharibika hatua kwa hatua, mifupa huanza kusuguana. Wakati huohuo mifupa mipya inayotokeza huanza kukua karibu na kiungo. Uvimbe unaweza kutokea, na mfupa ulio chini ya gegedu huwa mzito na kuharibika umbo.

Dalili nyingine za ugonjwa huo ni, vinundu kwenye viungo vya vidole, sauti ya kusugua katika viungo vilivyoathiriwa, mishtuko ya ghafla ya misuli, na vilevile maumivu, kukakamaa, na kushindwa kusogeza viungo. Zamani ilidhaniwa kwamba ugonjwa huo ulitokea tu kwa sababu ya uzee. Hata hivyo, hakuna uthibitisho wowote kwamba kiungo cha kawaida kinachofanya kazi ya kawaida tu kitaharibika katika kipindi cha maisha.

Wengine wanaoweza kupata ugonjwa huo ni watu ambao wana kasoro fulani katika viungo vyao, au wale wenye misuli dhaifu ya miguu na mapaja, miguu isiyo na urefu sawa, au kasoro katika uti wa mgongo. Wananawake wa makamo na wanawake wazee walio na watu wa ukoo wenye ugonjwa huo wanakabiliwa na hatari ya kuupata.

MATIBABU

Matibabu ya yabisikavu kwa kawaida huhusisha kutumia dawa, mazoezi ya mwili, na kubadili namna ya kuishi. Huenda tabibu wa maungo akaanzisha matibabu ya mazoezi ya mwili. Mazoezi hayo yanaweza kuhusisha mazoezi ya kukaza misuli, mazoezi yanayoboresha mfumo wa kupumua na mzunguko wa damu, kama vile kutembea au kukimbia, na mazoezi ya misuli ya kuinua vitu vizito. Mazoezi hayo yamesaidia sana kupunguza dalili nyingi kama vile uvimbe na maumivu ya viungo, unyong’onyevu, uchovu, na kushuka moyo.

Mazoezi yanaweza pia kuzuia kudhoofika kwa mifupa. Kupunguza unene kunaweza kusaidia sana kutuliza maumivu ya viungo yanayosababishwa na yabisikavu. Chakula kinachoweza kupunguza unene na vilevile maumivu ni mboga, matunda, na samaki wanaoishi katika bahari zenye maji baridi na mafuta mengi inayoitwa omega-3. Chakula kilichotayarishwa katika viwanda na chakula chenye mafuta yenye asidi nyingi kiepukwe. Vyakula vinavyotengenezwa kwa maziwa, ngano, na jamii ya mboga za mtunguja, nyanya, viazi, pilipili, na biringani husaidia kutibu.

Baadhi ya wagonjwa hutibiwa kwa kufanyiwa upasuaji unaohusisha kuingiza chombo fulani ndani ya kiungo chenyewe, na kuondoa utando unaotokeza vimeng’enya vinavyoharibu gegedu. Hata hivyo, mara nyingi uvimbe hurudi baada ya upasuaji huo.

Upasuaji wenye matokeo ya mara moja unahusisha kuondoa kiungo kizima (mara nyingi nyonga au goti) na kuweka kiungo kingine cha bandia.) Mara nyingi maumivu huisha kabisa baada ya upasuaji huo, na viungo vya bandia hudumu kwa miaka 10 hadi 15. Zipo dawa ambazo husaidia kutibu ugonjwa huu.


Loading...

Toa comment