Mtaalam Mandai
MALARIA ni maambukizi ya seli nyekundu za damu inayosababishwa na vimelea vinavyoitwa kitaalamu, Plasmodiumu.
Plasmodiumu hawa husambazwa na mbu aina ya Anofelesi. Mbu hutoa parasiti za malaria na kukomaa katika seli nyekundu za damu na mamilioni ya parasiti hukusanyika katika plasenta ya mjamzito. Malaria ni hatari zaidi kwa wajawazito kuliko watu ambao hawana mimba.
DALILI ZA MALARIA
Mama mjamzito anakuwa na dalili kama wagonjwa wengine ambao siyo wajawazito ambapo atajisikia baridi na kutetemeka, maumivu ya kichwa, mwili kuwa na joto kali, kutokwa na jasho joto lishukapo, kuhara au kutapika au kuwa na maumivu ya misuli au viungo.
VIPIMO VYA MALARIA
Malaria huweza kugundulika kwa kutumia vipimo vya haraka au darubini.
MATIBABU KWA MJAMZITO
Ni muhimu kwa wajawazito kuepukana na malaria – au kutibiwa haraka wakiwa wagonjwa. Dawa za kutibu malaria zinaweza kuwa na madhara, lakini ni afadhali kuliko kupatwa na malaria. Ikiwa mama ana dalili za malaria, anapaswa kutibiwa mara moja kwa kumuona daktari.
Wiki 12 za awali za ujauzito mama akiwa na malaria atatibiwa kwa Kwinini na Clindamycin au Kwinini pekee iwapo Clindamycin haipatikani. Dawa hizi zikishindwa kutibu Artesunate hutumika katika matibabu kwa muda wa siku saba.
Lakini dawa mseto jamii ya Artemisin zinaweza kutumika kutibu malaria ambayo siyo kali.
Mjamzito aliye na malaria anaweza kupata madhara kwa kuharibika mimba, kuzaa njiti, kuzaa mtoto aliyekufa au kufa yeye mwenyewe.
KINGA: Mjamzito afanye kila awezalo kuepuka kuumwa na mbu kwa kutumia chandarua, kupuliza dawa au kuua na kuangamiza mazalia ya mbu hupunguza au kuchoma dawa ya kuua mbu.