The House of Favourite Newspapers

Ugonjwa wa UTI kwa wajawazito -2!

MAAMBUKIZI ya njia ya mkojo (UTI) husababishwa na vimelea ambavyo kitaalamu hujulikana kama E. Coli. Vimelea hawa huishi kwenye mfumo wa chakula bila kuleta madhara yoyote wawapo humo, ila wakiingia kwenye njia ya mkojo huleta maambukizi na kusababisha ugonjwa wa UTI.

Kutokana na sababu za kimaumbile, wanawake huathirika zaidi na ugonjwa wa UTI kuliko wanaume, hii ni kwa sababu kuna ukaribu zaidi katika njia hizi mbili za chakula na mkojo. Na pale mtu anaponawa baada ya haja kubwa, ni rahisi zaidi kuhamisha vimelea hivi vya E. Coli kwenye njia ya mkojo pale ambapo hujifuta kuelekea mbele. Ndiyo maana kwa wanawake hushauriwa kunawa kuanzia mbele kuja nyuma. Endapo utanawa kuanzia nyuma kuja mbele, kuna uwezekano wa kuhamisha vimelea hivi ambavyo husambaa hadi kwenye kibofu na endapo hautatibiwa vyema, basi hupanda hadi kwenye figo.

Pia, wanawake huathiriwa sana na UTI kwa sababu wana njia nyembamba ya mirija ya mkojo ambayo inawapa bakteria wa UTI urahisi wa kusafiri hadi kwenye kibofu cha mkojo. Kujamiiana pia kunaweza kupelekea kupata bakteria wanaosababisha UTI.

Dalili za maambukizi ya njia ya mkojo

>Maumivu wakati wa haja ndogo, na hisia ya mkojo kuchoma choma

>Kubanwa na mkojo mara kwa mara

>Maumivu ya kiuno na maumivu ya chini ya kitovu

>Mkojo wa njano sana na muda mwingine unatoa harufu

>Uchovu

>Homa

>Kichefuchefu na kutapika

Unapohisi dalili hizi ni vyema kwenda kwa daktari ili upate tiba muafaka badala ya kuanza kutumia madawa bila ya mpangilio maalumu, kitu kitakachoweza kukusababishia kukomaza ugonjwa. Pia, kuna baadhi ya dalili za UTI hufanana na zile za magonjwa ya zinaa hivyo, vipimo vya maabara huhitajika kuweza kutambua kama unachoumwa ni UTI au ni magonjwa ya zinaa (STD)

Vipimo:

>Kupima mkojo kuangalia kama kuna chembechembe nyeupe na vimelea

>Kuotesha mkojo kuangalia vimelea

>Ultrasound ya tumbo chini ya kitovu kuangalia njia ya mkojo na hasa kibofu

Jinsi ya kujikinga na maambukizi ya njia ya mkojo

>Kunywa maji mengi

>Baada ya haja kubwa ni vizuri kunawa kuanzia mbele kurudi nyuma

>Pendelea kwenda kukojoa pindi unaposikia umeshikwa na mkojo na hakikisha umetoa mkojo wote.

>Hakikisha sehemu za siri zipo safi kabla ya kujamiiana

>Ni vizuri kupata haja ndogo mara baada ya kujamiiana ili kusafisha bakteria ambao wanaweza kuwepo kwenye njia ya mkojo,

Hakikisha sehemu za siri zipo kavu, pendelea kuvaa nguo za ndani zilizotengenezwa kwa pamba, pia zenye kuacha unafasi, epuka jinzi zinazobana au nguo za ndani za nailoni kwa sababu zitapelekea kuwa na hali ya unyevunyevu na kuleta mazingira rafiki kwa ukuaji wa bakteria.

UTI kwa wajawazito

Wanawake wajawazito wapo kwenye hatari ya kupatwa na ugonjwa wa UTI. Homoni wakati wa ujauzito hupelekea kutokea mabadiliko kwenye njia ya mkojo. Pia, uterus huongeza mgandamizo kwenye mishipa inayopitisha mkojo kutoka kwenye kibofu na kibofu chenyewe, hali hii husababisha mkojo kupita kwa shida kutoka kwenye figo kuja kwenye kibofu au kutoka kwenye kibofu chenyewe. Mambo ya kuzingatia ni kama nilivyoeleza hapo juu.

Comments are closed.