The House of Favourite Newspapers

Ugumu/urahisi wa kufanikiwa na msemo wa ‘one day yes’

0

Ndugu zangu, maisha ya sasa yamekuwa yakitafsiriwa tofauti na kila mtu. Wapo wanaoeleza kuwa, maisha ni magumu, maisha ni yenye upendeleo na kuongeza kuwa maisha hayana haki.
Wanaokuwa na dhana hizo potofu wanafikia hatua ya kukata tamaa kabisa na kuridhika kuishi maisha yasiyo na mbele wala nyuma.

Wapo watu huko mtaani ambao wana afya nzuri, nguvu za kutosha lakini wamekata tamaa ya maisha kiasi cha kuridhika kabisa kuishi kifukara na hata kufikia hatua ya kula mlo mmoja tu kwa siku. Hawa ukiwauliza wanasema maisha ni magumu!

Lakini wakati hao wakisema hivyo, wapo wanaoamini kwamba hakuna aliyeletwa hapa duniani ili aishi kwa tabu. Watu hawa wanaongozwa na imani ya kwamba, kila mtu anaweza kuishi maisha mazuri yaliyotawaliwa na furaha kama ataamua. Kila mtu anayo nafasi ya kuwa na mafanikio makubwa kama ataweka dhamira hiyo mbele.

Ikumbukwe umaskini upo na maskini haiwezi kuwa miti wala wanyama, ni binadamu na upo ili kuwa mwanzo wa kuelekea kwenye utajiri. Huwezi kutoka kwenye utajiri ukaingia kwenye utajiri bali lazima uanze kwenye umaskini kisha ndiyo uelekee kwenye utajiri. Labda tu kwa wale ambao wamerithi utajiri kutoka kwa ndugu zao.

Nikuambie kitu kimoja ndugu yangu kwamba, kama unataka kuwa mbali na umaskini lazima ufanye kazi kwa bidii zote na upingane na mazingira yoyote yanayoweza kukusababishia kuishi maisha duni.
Unaweza kuona ugumu wa wewe kuwa kati ya waliofanikiwa kutokana na jinsi ulivyo sasa lakini niamini mimi, wapo ambao walikuwa maskini wa kutupwa lakini wakaona hawastahili kuwa hivyo, wakapambana na leo hii ni watu wa tofauti kabisa.

Umaskini kwao imebaki historia, tena historia yenye fundisho kwa wengine kwamba kumbe inawezekana kuwa tajiri kama utaamua.
Ndiyo maana nasema kuwa, wakati bado uko hai na Mungu amekujaalia afya njema, nguvu na maarifa, amini ukiwa na dhamira ya dhati kabisa ya kufanikiwa, kuna siku ndoto hiyo itatimia.
Inaweza ikawa siyo leo, kesho wala keshokutwa lakini ipo siku utakaa kivulini na kujipongeza kwa mafanikio uliyoyapata.

Mifano ya watu waliopitia katika hiki ninachokieleza ipo huko mtaani. Yupo kijana ambaye niliongea naye mwaka juzi mwishoni. Alikuja Dar akitokea Dodoma, akawa anafanya kazi sokoni Kariakoo. Kwa bahati mbaya kila alichokuwa akifanya, faida alikuwa haoni.

Akakata tamaa, akahisi njia pekee ni kurudi kwao kulima. Siku moja alisoma moja ya makala zangu, akanipigia simu, nikamshauri na kumtia nguvu.Nilimweleza hayahaya kwamba, mafanikio hayaji haraka kama alivyokuwa akifikiria.

Utajaribu, utashindwa, utajaribu tena utashindwa, ukikata tamaa katika mazingira hayo utakuwa umekataa mafanikio lakini ukiendelea kupambana, siku moja mambo yatakunyookea.
Maneno hayo yalimpa ujasiri na leo hii ninavyoandika makala haya ni moja kati ya wafanyabiashara wakubwa sokoni Kariakoo. Na wewe pia kuwa na subira, vumilia na pambana, wazungu wanasema ‘one day yes’, yaani siku moja mambo yatakunyookea.

Leave A Reply