The House of Favourite Newspapers

UJUE MPANGO KUUNGANA KWA WHATSAPP, FACEBOOK & INSTAGRAM

 

FACEBOOK ina mipango ya kuunganisha huduma zake za kutuma ujumbe katika Instagram, WhatsApp na Facebook Messenger.

 

Licha ya kwamba huduma zote tatu zitasalia kuwa programu huru, zitashirikiana kupitia ujumbe utakaotumwa kutoka huduma moja hadi nyingine.

 

Facebook imeliambia shirika la utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba huo ndiyo mwanzo wa mchakato mrefu.

 

Mpango huo kwanza uliripotiwa mjini New York na unaaminika kuwa mradi wa kibinafsi wa mwanzilishi wa Facebook, Mark Zuckerberg.

 

Utakapokamilika, ushirikiano huo utamaanisha kwamba mtumiaji wa Facebook anaweza kuwasiliana moja kwa moja na mtu ambaye anamiliki akaunti ya WhatsApp.

 

Hili haliwezekani kwa sasa kwa kuwa programu zilizopo hazina uhusiano.

 

Hatua ya kuunganisha huduma hizo tatu imeanza, kulingana na gazeti la The New York Times,  na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2019 ama mapema mwaka ujao.

 

 

Facebook haikupendelea kuzungumzia suala hili katikati ya kashfa iliyoikumba, lakini ililazimishwa na watu waliokuwa wakiwasiliana na New York Times.

 

Hadi kufikia sasa, WhatsApp, Instagram na Messenger zimekuwa zikifanya kazi kivyake na kushindana kibiashara.

Kuunganisha huduma hizo kwa kutuma ujumbe kutarahisisha kazi ya Facebook.

 

Haitalazimika kuunda programu mpya kama vile ‘stories’ ambapo huduma zote tatu zimeongeza katika programu yake bila mafanikio ya kufurahisha.

 

Mawasiliano ya ujumbe kupitia huduma moja hadi nyingine yanaweza kuimarisha biashara katika huduma moja kwa kutuma ujumbe kwa huduma nyingine.

 

Pia yatairahisishia Facebook kugawana data katika huduma zote tatu ili kusaidia juhudi za matangazo yake.Hatua hiyo pia itaimarisha uwepo wa Facebook na kuwa vigumu kuanguka iwapo serikali husika zitajaribu kuivunja kwa manufaa yao ya kibinafsi.

 

Zuckerberg ameripotiwa kushinikiza ushirikiano huo ili kuimarisha huduma za kampuni yake kuwa muhimu na kuongeza muda wa wakati unaotumika na wateja wake katika huduma hizo.

 

 

Kupitia kuunganisha wateja wake katika kundi moja kubwa, Facebook itaweza kushindana vizuri na kampuni ya Google na Apple iMessage kwa mujibu wa Makena Kelly wa mtandao wa habari wa The Verge.

 

“Tunataka kuunda huduma bora zadi ya kutuma ujumbe iliyo na ulinzi wa hali ya juu na kufanya kuwa rahisi kuwafikia marafiki na familia kupitia huduma tofauti,”  aliongezea.

 

Taarifa hiyo ilisema kuwa kulikuwa na majadiliano na mjadala kuhusu vile mfumo huo utakavyofanya kazi.Kuunganishwa kwa huduma hizo tatu kutaleta mabadiliko muhimu katika kampuni ya Facebook kwa kuwa imeruhusu Instagram na WhatsApp kufanya kazi kama kampuni tofauti zilizo huru.

 

Gazeti la The New York Times linasema kuwa hatua ya Zuckerberg kupigania mpango huo wa kuunganisha huduma hizo umesababisha mgogoro wa ndani.

 

Inadaiwa ndiyo sababu ya waanzilishi wenza wa Instagram na WhatsApp kuondoka mwaka uliopita.Hatua hivyo inajiri huku Facebook ikikabiliwa na uchunguzi na kukosolewa kuhusu  inavyotunza data za wateja wake.

 

JIUNGE NA FAMILIA YA GLOBAL TV UPANDE MTANDAO WA MAFANIKIO

Bofya hapa kujiunga na familia ya Global TV Club ==> Global TV Family Club

 

Comments are closed.