The House of Favourite Newspapers

Ujue ugonjwa hatari wa wanawake

UGONJWA uitwao Endometriosis ni ugonjwa hatari ambao wanawake wengi hawaujui lakini unasababishwa na tishu zinazotengeneza ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi kukua sehemu ya nje ya mfuko wa uzazi.  Sehemu ya ndani ya ukuta wa mfuko wa uzazi huitwa “endometrium” kwa lugha ya kitaalamu na ugonjwa wa Endometriosis hutokea wakati ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi unapokuwa juu ya mfuko wa mayai ya uzazi kitaalamu huitwa ovary, utumbo na tishu zilizopo kwenye mifupa ya kiuno yaani pelvis.

Si kawaida kwa tishu za endometrial kuenea zaidi ya eneo la mifupa ya kiuno na huwa haiwezekani kutokea. Tishu zinazokuwa ndani ya ukuta wa mfuko wa uzazi (Endometrial) na zinazoota au kukua nje ya mfuko wa uzazi au kwa jina lingine mji wa mimba huitwa “endometrial implant” kwa lugha ya kitaalamu, hali hiyo inaweza kusababisha mwanamke asishike mimba. Mabadiliko ya homoni ya mzunguko wa hedhi wa mwanamke husababisha kubadilishwa kwa tishu za ukuta wa mfuko wa uzazi. Hii ina maana kwamba tishu hiyo hukua, hukomaa, na kuvunjika.

Baada ya muda, tishu iliyovunjika huelekezwa maeneo ya mifupa ya kiuno (pelvis) na kubakia mahali hapo. Tishu zilizonyakuliwa na eneo la mifupa ya kiuno (pelvis) husababisha yafuatayo; maumivu makali ya kuchoma sehemu ya kiuno, hivyo wanawake wanaougua kiuno wanapaswa kwenda kupimwa kwa mtaalamu wa afya.

Pia tishu hizo zilizonyakuliwa na eneo la mifupa ya kiuno (pelvis) husababisha makovu maeneo ya uzazi. Tishu hizo hushikanisha viungo vilivyopo maeneo ya mifupa ya kiuno (pelvis) na maumivu makali kutokea hasa wakati wa hedhi. Tishu hizo pia husababisha matatizo ya uzazi na mwanamke kukosa uwezo wa kushika mimba.

DALILI ZA UGONJWA

Dalili za ugonjwa huu hatari ni mwanamke  kusikia maumivu makali ya kuchomachoma kiunoni, maumivu makali kabla au baada ya hedhi, maumivu makali wakati wa tendo la ndoa na maumivu ya tumbo. Dalili nyingine ni maumivu kwenye mgongo na maeneo ya mifupa ya kiuno (pelvis), maumivu unapotaka kwenda kujisaidia/kwenda haja na  maumivu ya miguu.

Mwanamke pia anaweza kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi, damu hiyo inaweza kuwa au kutokuwa na mabonge. Anaweza kuwa na hedhi ya muda mrefu isivyo kawaida na anaweza kupata hedhi kabla ya muda wa kawaida.

Anaweza pia kupata maumivu makali wakati wa tendo la ndoa, kuwa na matatizo ya kibofu na tumbo na kutokwa na damu maeneo ya kibofu au tumboni. Mwanamke anaweza kupata haja kubwa ngumu (constipation), kuharisha, kukojoa  mara nyingi isivyo kawaida na kuvimba kwa tumbo wakati wa hedhi na kuambatana na maumivu lakini pia anaweza asisikie maumivu.

TIBA, USHAURI

Uonapo dalili hizo hasa maumivu ya kiuno kwa kuchomachoma au kuumwa mgongo au kukojoa damu, muone mtaalamu wa afya ambaye atakupima na akigundua tatizo, atakupa dawa ambazo zitakutibu na kumaliza tatizo.

Ugonjwa huu ni hatari kwani licha ya mgonjwa kupata maumivu, mwanamke asipotibiwa mapema unaweza kusababisha matatizo katika mji wa uzazi, hivyo kumsababishia mwanamke kutoshika mimba.

Comments are closed.