Ujumbe wa Papa Leo XIV Siku ya Amani Duniani 2026, Kuhusu Vita, Silaha na Amani ya Kweli

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo, amesisitiza kuwa amani si ndoto wala kauli ya kiimani pekee, bali ni haki ya msingi ya binadamu na nguzo kuu ya kulinda utu wa mwanadamu, akionya kuwa dunia inaelekea kupoteza mwelekeo wa kimaadili kwa kuhalalisha vita, matumizi ya nguvu na uwekezaji mkubwa wa kijeshi.
Katika ujumbe wake wa kurasa nne uliotolewa kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani ya Kanisa Katoliki, Papa Leo amesema kuwa kauli ya kale “Amani iwe nanyi” si salamu tu, bali ni mwito wa mageuzi ya kina yanayogusa dhamira, sera na maamuzi ya jamii na mataifa.
Kwa mujibu wa Papa Leo, ongezeko la matumizi ya kijeshi duniani lililofikia dola trilioni 2.7 mwaka 2024 linadhihirisha kipaumbele kinachotolewa kwa silaha badala ya maisha ya watu, huku haki za raia, ustawi wa kijamii na diplomasia vikisukumwa pembeni.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Leo XIV
Siku ya 59 ya Amani Duniani – 1 Januari 2026
Kaulimbiu: Kuelekea amani “isiyo na silaha na inayopokonya silaha”
1. “Amani iwe nanyi”
Baba Mtakatifu anakumbusha kuwa salamu ya Yesu Mfufuka “Amani iwe nanyi” si maneno tu, bali ni nguvu hai inayobadilisha mioyo na ulimwengu. Amani ya Kristo ni ya unyenyekevu, uvumilivu, isiyo na silaha na inayopokonya silaha, kwa kuwa chanzo chake ni Mungu anayewapenda wote bila masharti.
2. Kristo ni Amani Yetu
Yesu, Mchungaji Mwema, alivunja kuta za migawanyiko na kushinda kifo. Ingawa dunia inaonekana kujaa giza, amani bado ipo na inataka kukaa ndani ya kila moyo wa binadamu. Amani hushinda vurugu, huleta mwanga, na hufungua njia ya matumaini hata katikati ya vita na hofu.
3. Amani si ndoto, ni safari
Papa anasisitiza kuwa amani si lengo la mbali bali ni uwepo unaoishiwa na safari ya pamoja. Hata pale ambapo kuna magofu na kukata tamaa, bado kuna watu wanaoshuhudia amani kwa matendo yao. Amani huongoza maamuzi yetu na hutuita kuchagua wema, pamoja na wengine.
4. Amani Isiyo na Silaha
Yesu alikataa kujilinda kwa nguvu za silaha na aliwaambia wanafunzi wake waache upanga. Huu ni msingi wa Ukristo: kupinga vurugu kwa njia ya huruma na upendo. Papa anakemea mantiki ya dunia inayohalalisha vita, mashindano ya silaha na hofu, hasa matumizi ya silaha za nyuklia.
5. Hatari ya ulimwengu wa leo
-
Matumizi ya kijeshi yanaendelea kuongezeka duniani
-
Elimu na mawasiliano yanazidi kuhalalisha fikra za vita
-
Teknolojia mpya, hususan akili unde (AI), zinahatarisha heshima ya maisha ya binadamu kwa kuhamisha maamuzi ya uhai na mauti kwa mashine
Haya yote ni tishio kubwa kwa utu wa binadamu na mustakabali wa ustaarabu.
6. Amani Inayopokonya Silaha
Papa anakumbusha kuwa wema hupokonya silaha. Mungu alikuja kama mtoto dhaifu, akifunua nguvu ya upendo na unyenyekevu. Amani ya kweli huanza kwa kupokonya silaha za mioyo, kuondoa hofu, chuki na tamaa ya kutawala wengine.
7. Jukumu la Dini na Jamii
Dini zina wajibu wa:
-
Kukataa matumizi ya jina la Mungu kuhalalisha vurugu
-
Kukuza sala, mazungumzo ya kiekumeni na ya dini mbalimbali
-
Kujenga jumuiya zinazokuwa “nyumba za amani”
Wakati huo huo, diplomasia, sheria za kimataifa na taasisi za juu za kimataifa zinapaswa kuimarishwa, si kudhoofishwa.
8. Tumaini kwa Dunia
Papa anahitimisha kwa wito wa tumaini, hasa katika Mwaka wa Jubilei ya Tumaini. Amani inawezekana ikiwa binadamu wataanza na mageuzi ya ndani ya mioyo, akili na maisha. Ndipo ahadi ya Mungu itatimia:
“Watafua panga zao ziwe majembe… taifa halitainua upanga dhidi ya taifa lingine tena.”
Soma BONYEZA Hapa >>>>Ujumbe wa Papa Leo XIV Siku ya Amani Duniani 2026

