The House of Favourite Newspapers

Ukatili ulioje! Shangazi amchoma mkono mtoto wake

0

Ukatili-(1)Mtoto Dorine anayedaiwa kuchomwa mikono na shangazi yake.

Ni ukatili ulioje ambao amefanyiwa mtoto Dorine (12), denti wa darasa la nne Shule ya Msingi Makabe, Mbezi jijini Dar.

Dorine anadaiwa kuunguzwa na maji ya moto yaliyochemshwa kwenye jiko la gesi na walezi wake wa karibu akiwemo shangazi yake aliyetajwa kwa jina moja la Scola ambaye alitiwa mbaroni na bibi yake ambaye haikujikana alipo.

Ukatili-(3)Katika tukio hilo la Septemba 26, mwaka huu, Scola alidaiwa kutekeleza tendo hilo, chanzo kikielezwa ni upotevu wa shilingi 20,000.

Kwa mujibu wa chanzo makini, Scola alimtaka Dorine aseme amezipeleka wapi fedha hizo, lakini binti huyo alisema hajui chochote.

Ilidaiwa kwamba, katika hali isiyokuwa ya kibinadamu, wakati Dorine akiwa anahojiwa tayari maji ya moto yalikuwa yakichemka.

ukatili
Ilisemekana kwamba, baada ya kuona Dorine hataki kusema zilipo fedha hizo, Scola akamuamuru aingize mikono ndani ya sufuria lililokuwa jikoni huku maji yakichemka.

Dorine alipokataa, Scola akadaiwa kumshika kwa nguvu, akisaidiana na mama yake ambaye ni bibi wa Dorine na kuizamisha kwenye sufuria la maji mikono hiyo na kumsababishia mtoto huyo majeraha ya kutisha.

Ilisemekana kwamba, baada ya tukio hilo, familia hiyo ilifanya siri kubwa na kutompeleka hospitalini lakini baadhi ya majirani walibaini hilo na kusambaza taarifa ndipo familia hiyo ikampeleka hospitalini kwa siri.

Alipofikishwa katika Hospitali ya Kanisa Katoliki Luguruni, Mbezi mtoto huyo alilazwa baada ya mahojiano na wauguzi ambapo aliwaeleza kila kilichotokea.

Hata hivyo, maelezo ya Dorine kwamba aliunguzwa na shangazi na bibi yake yalipingwa na Scola ambaye alisema mtoto huyo alikuwa akikimbia akaangukia maji ya moto.

Taarifa alizopata mwanahabari wetu kwenye hospitali hiyo kupitia muuguzi wa zamu, zilieleza kuwa taarifa sahihi za tukio hilo ni zile alizozitoa mtoto  huyo.

Katika mahojiano na wauguzi, Dorine ambaye alikuwa amelazwa kwenye Chumba cha Stuff Na. 16 hospitalini hapo, alifafanua kuwa anaishi kwa shangazi yake  baada ya baba yake mzazi kuachana na mama  yake na baba kuoa mwanamke mwingine.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili ulibaini kwamba, Scola alishikiliwa na Jeshi  Polisi Kituo cha Mbezi-Kwayusuf na baadaye aliachiwa kwa dhamana lakini bibi hakukamatwa.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, RPC Camilius Wambura alipoulizwa na gazeti hili juu ya tukio hilo alikiri kulijua na kwamba alipokea taarifa za aina mbili hivyo alimwagiza OCD wa Mbezi-Kwayusuf kulifuatilia na kumpa taarifa kamili.

Alisema taarifa moja ilidai, Dorine aliunguzwa lakini ya pili ilidai aliangukia kwenye sufuria yenye maji ya moto hivyo uchunguzi unaendelea ili kupata taarifa kamili.

Leave A Reply