BINALONAN kijiji kinachopatikana kaskazini mwa mji mkuu wa Ufilipino, Manila, kimepiga marufuku kufanya umbea. Meya wa mji, Ramon Guico, amesema umbea ulisababisha ugomvi mkubwa utokee katika kijiji hicho, kitu kilichosababisha vikao vya viongozi kuchukua tahadhari kwa kupiga marufuku umbea.
Guico alisema kuna umbea wa aina nyingi, lakini katika kijiji hicho kesi nyingi ni za umbea unaohusu mali, pesa na mahusiano. Sababu ya marufuku hiyo ni kukumbusha kwamba kila mtu na hasa wanaoishi katika kijiji hicho, anawajibika kwa atakayoyasema.
Pia wanataka kuwaonyesha watu wengine kwamba watu wa Binolonan ni watu wazuri na eneo hilo ni salama. Guico, aliongeza kwamba hatua walizochukua zitaongeza ubora wa kijiji hicho. Guico aliongeza kwamba maeneo ambayo watu wake hawafanyi umbea yana baraka zaidi, kwa sababu yeye anaamini watu wana kazi muhimu zaidi za kufanya badala ya kufanya umbea.
Kwa mujibu wa sheria, atakayekutwa na hatia ya kufanya na kueneza umbea na maneno ya uongo, atatozwa faini pesa taslimu peso 200 takribani Dola za Marekani 4. Pamoja na tozo hilo la pesa, atapewa adhabu ya kukusanya takataka kwa saa tatu.
Atakayekutwa na hatia ya kufanya umbea kwa mara ya pili atatozwa faini ya pesa taslimu peso 1,000 takribani Dola 20, na faini hiyo itaambatana na kupewa adhabu ya kutoa huduma kwa jamii kwa saa nane.
Comments are closed.