UKIMCHAGUA MWENZA KWA STAILI HII, IMEKULA KWAKO!

NI wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii nikiamini kwamba Mungu ameendelea kukupa ulinzi. Pia niwatakie kila la heri waislam ambao sasa hivi wako kwenye kuumaliziamalizia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.  Mpenzi msomaji wangu, uhusiano wa kimapenzi siku zote unajengwa na imani. Wapendanao wanapaswa kuaminiana kwa asilimia mia. Waswahili wanakwambia bora ukosee njia lakini usikosee kuoa. Msemo huu una maana kubwa sana katika maisha ya kila siku, dunia ya sasa imejaa changamoto za kila aina. Ubinadamu uliokuwepo enzi za mabibi na mababu zetu umepotea. Binadamu wanafanya mambo kama wanyama.

Ukiingia kwenye uhusiano na mtu ambaye si sahihi, ni dhahiri utakuja kupata tabu sana huko baadaye. Unaweza kuingia kwenye uhusiano na mtu ambaye hana huruma, hajali na wala hana hekima hivyo mtakapokuja kuingia kwenye ndoa, utashuhudia balaa lake. Maisha ya wapendanao yanatengenezwa na upendo, kuna watu ni wanandoa lakini unakuta mke hana upendo hata kidogo wa mumewe. Au unakuta mume hana upendo hata kidogo kwa mkewe, hili husababisha msuguano wa hali ya juu katika safari.

Ndugu zangu, ndoa ni muunganiko ambao Mungu aliuweka ili mwanamke na mwanaume kweli washibane katika kila hali. Mpendane katika shida na raha, katika uzima na ugonjwa. Sio unaingia kwenye ndoa na mtu katili, hana utu mtu wa aina hiyo ni hatari sana.

Kwa kawaida, vijana wengi wa sasa hukosea katika suala zima la kuingia kwenye urafiki, uchumba na hata ndoa. Tamaa za kimwili ndizo zinazowaongoza kuchangua wenzi wao wa maisha badala ya utu, ubinadamu, hekima na busara. Mtu anaangalia shepu ya mtu. Anaangalia uzuri wa mtu kimuonekano bila kujua, mtu huyohuyo mwenye muonekano wa kuvutia, muonekano wa kumpendeza kila mtu anaweza kuwa sumu hatari sana katika maisha yake.

Anaingia na mtu kwenye uhusiano ambaye ni kirusi hatari ambacho kiko tayari hata kumuua kwa ajili tu ya masilahi fulani. Mwisho wa siku anajikuta akikumbana na unyama wa hali ya juu ambao hakuna anayeweza kukubaliana nao pindi utakapomhadithia. Ndugu zangu, tunapaswa kuwa makini sana pindi tunapofanya maamuzi ya wenza wa maisha. Tusikurupuke, tutulize sana akili zetu kabla ya kufanya maamuzi. Tutumie akili zetu za kibinadamu. Tutazame na kumpima mtu kwa mambo mengi kabla ya kufanya maamuzi.

Unayetaka kuanzisha naye safari, ana mapenzi ya dhati? Ana moyo wa kusamehe? Ana hofu ya Mungu? Ana utu, historia yake ikoje? Wengi wetu huwa hatumsomi mtu historia yake. Unakutana na mtu klabu, unakutana na mtu baa halafu unafanya maamuzi ghafla, mnaingia kwenye uchumba na ndoa.

Muhimu hapa ndugu zangu ni kumsoma mtu, kuwa naye kwenye urafiki, uchumba na katika kipindi hicho japo watu huwa wanabadilika lakini angalau inaweza kukusaidia kukupa picha kwamba upo na mtu wa aina gani. Pamoja na macho yetu, mtangulize Mungu katika hilo. Muombe Mungu akupe mtu sahihi, muombe yeye akuoneshe maana wakati mwingine akili zetu zinatuzuzua.

 


Loading...

Toa comment