Ukiolewa ilimradi umeolewa, baadaye itakukosti

Couple-in-BedNI Mungu pekee anayestahili kusujudiwa, kwa rehema zake nimepata nafasi ya kuzungumza nawe tena msomaji wangu kupitia safu hii.

Mada ya leo itajikita zaidi kwa baadhi ya watu kukimbilia kuolewa ilimradi tu na wao waweke kumbukumbu akilini mwa watu kuwa walishawahi kuolewa. Ndoa hizi mara nyingi zinawakosti wengi.

Ndoa siyo kitu cha kukimbilia, kupapatikia, kung’ang’ania, ndoa ni mpango wa Mungu ambao huufanya kwa kuwaunganisha wanadamu wa jinsi mbili tofauti ambao wameridhiana wao na kuwashirikisha jamaa zao.

Baadhi ya watu wamekuwa wakitamani kuolewa na f’lani kwa sababu tu ana kitu f’lani au ukoo wao ni watu wenye elimu sana, akili au uwezo wa juu. Kuchagua ukoo unaotaka kwenda kuoa au kuolewa siyo jambo baya, kwani hata miaka ya 1970 kwenda nyuma, kijana alikuwa anachaguliwa kwa kwenda kuoa au kuolewa na alichaguliwa kwa sababu ya tabia ya familia lengwa na siyo kwa sababu wana mashamba mengi, mifugo mingi au wana uwezo wa aina yoyote ile, kikubwa kilichaoangaliwa ni tabia ya familia hiyo.

Lakini ukija katika kizazi hiki cha WhatsApp hali ni tofauti, mwanamke anataka kuolewa na jamaa kwa sababu ana jina kubwa mtaani au umaarufu wake mjini pasipokujua tabia za asili na vigezo vinavyomfanya kuwa maarufu.

Kwa mantiki hiyo wanawake wengi wamekuwa wakiangukia pabaya kwa kuolewa na watu wasiowapenda kwa dhati toka mioyoni mwao.

Mara nyingi ndoa za namna hiyo huwajutisha wanandoa baadaye hasa upande wa wanawake kwani inafika sehemu mwanamke anatamani kujinasua kwenye ndoa hiyo kwa sababu tu imegeuka mateso kwake, lakini inashindikana.

Kama hujaingia kwenye ndoa nakuomba ujitahidi sana kumshirikisha Mungu akupe maono au jicho la tatu kuweza kubaini ndoa na mtu sahihi wa kuwa naye ili baadaye isije ikakukosti.

Usiolewe kwa sababu tu unataka kuolewa kwa sababu mashoga zako wote wameolewa, eti kisa wewe ni msichana mkubwa kwenu ambaye hujaolewa huku wadogo zako wameolewa na wana watoto. Ndoa haitaki hivyo, funga na uombe usije ukaangukia pabaya.

Napenda kukuhakikishia kuwa kama utaolewa kwa sababu ya kutimiza wajibu wa kuolewa au kufuata vitu nilivyovisema awali, hutadumu kwenye hiyo ndoa, kwani kuna wakati hata tendo la ndoa utakuwa unaona hustahili kushiriki na mwenza wako inakuwa kama anakubaka kwani hujisikii raha tena kama zamani. Mapenzi ni matamu, yana raha kama utampata mtu sahihi na siyo kwa  mtazamo wa mali au cheo chake.

Ni hayo tu! Usikose kutembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta: mimi_na_uhusiano au unaweza kujiunga kwenye group letu la WhatsApp kwa namba za hapo juu.


Loading...

Toa comment