The House of Favourite Newspapers

Ukiolewa, kuwa mshauri wa mumeo!

0

BLD080939Asalam Alaikum, Bwana Yesu asifiwe, bila shaka wasomaji wangu wa safu hii ni wazima na mnaendelea vema na ujenzi wa taifa kwa hilo nashukuru Mungu.

Leo nimekuja na mada mpya ambayo imenisukuma kuwaandikia wanawake wengi ambao wapo kwenye ndoa na hii imekuwa kama fasheni kwa ndoa nyingi jambo linalokera na wala halipendezi kwa ndugu ama jamii.

Wanawake wengi tunashindwa kuwashauri waume zetu jinsi ya kutumia pesa, tunaendekeza starehe na sehemu ambazo si za kutusaidia hapo baadaye.
Wiki iliyopita nilipokea ujumbe kutoka kwa msomaji mmoja ambaye alitoa malalamiko yake kwa mapito aliyopitia.

Anasema kuwa hadi sasa anajutia kupoteza muda wake kwani ameshaishi na wanawake zaidi ya wanne lakini wote aliachana nao kisa kikiwa ni kukosa ushauri mzuri walipokuwa wakiishi pamoja, hebu msikie;

“Mimi ni baba wa watoto wawili, nilikuwa katika uhusiano na wanawake wanne na wote niliachana nao kwa vipindi tofauti. Kwa upande wa kipato ninacho kizuri namshukuru Mungu lakini kitu kikubwa kilichonisukuma niwasiliane na wewe ni kwa jinsi nilivyohangaika katika mapito yangu.

“Mwanamke wangu wa kwanza ambaye nilizaa naye alikuwa mzuri na hakuwahi kunisaliti lakini tatizo lake kubwa alikuwa si mshauri mzuri kwangu na kwa watoto pia. Ushauri wake mwingi ulikuwa starehe na matumizi yasiyo ya msingi na wala hayakuwa katika kujenga familia.

“Niliamua kuachana naye na kukaa kipindi kirefu nikilea wanangu. Hadi sasa nimeshamaliza wanawake zaidi ya wanne na niliyempata hakika ni chaguo la Mungu kwani ana malengo mengi katika maisha, ni mtu wa kunishauri kwa kila nitakachokifanya,” alisema msomaji huyo.

Bila shaka mmenielewa nyie wanawake wenye tabia hii, kwanza unapata bahati ya kuolewa na mwanaume mwenye heshima na pesa zake, badala umshauri vitu vya msingi jinsi ya kuishi na kutumia pesa wewe unawaza starehe tu.

Labda nitoe ushauri kwa wanawake wenzangu wote mnaosoma mada hii leo, wakati mwingine tuwe kwanza na shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kubarikiwa kupata wanaume wa namna hii.

Mwanamke unatakiwa uwe mshauri kwa mumeo, usimfanye mwanaume wako aje kuwa masikini kwa kipindi ambacho pesa anazo lakini hajui atazitumiaje? Hapa ushauri unaopaswa kumpa ni kujenga, kufanya biashara, kununua mashamba na mengine mengi na siyo kuendekeza starehe.

Kwa leo naishia hapa tuonane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri…

Leave A Reply